Ben White akataa kuitwa kwenye kikosi cha England

Muktasari:

  • Southgate alitaja majina ya mastaa hao watakaocheza mechi za kirafiki dhidi ya Brazil na Ubelgiji jioni ya leo na akafafanua kwanini White hayupo.

LONDON, ENGLAND: Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate amesema beki wa Arsenal, Ben White hajajumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 kitakachoingia kambini kwa ajili ya mechi za kirafiki za kalenda ya FIFA kwa sababu amekataa mwenyewe.


Southgate alitaja majina ya mastaa hao watakaocheza mechi za kirafiki dhidi ya Brazil na Ubelgiji jioni ya leo na akafafanua kwanini White hayupo.


"Najua ni swali ambalo mtauliza, lakini siwezi kukaa hapa na kuwaambia kwamba hastahili kuwa kwenye timu ya taifa kwa sababu ameonyesha kiwango bora.

Tulipokea simu kutoka kwa Mkurugenzi wa Arsenal Edu, akatuambia kwamba White hahitaji kujumuishwa kwenye kikosi cha England kwa sasa.


"Ni aibu kwa sababu ni mchezaji ambaye nampenda sana, nilijaribu kuzungumza naye baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia kule Qatar 2022, nashangaa kuibuka haya, mwisho wa siku natakiwa niheshimu mawazo yake na kuacha mlango wazi ili aondoke, hayupo na sisi lakini hakuna shida yoyote baina yetu na yeye"


White aliondoka kwenye kambi ya England wakati michuano ya Kombe la Dunia inaendelea kule Qatar huku taarifa zikidai kwamba ni kwasababu zake binafsi lakini ripoti za ndani zikafichua kwamba aligombana na kocha msaidizi Steve Holland, lakini Southgate amekanusha taarifa hizo.


Tangu kuanza kwa msimu huu akiwa na Arsenal, White amecheza mechi 39 za michuano yote.