Beckham amnasa Casemiro Miami
Muktasari:
- Kwa mujibu wa mwandishi maarufu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano kupitia akaunti yake ya X, Casemiro alikuwa karibu kukamilisha uhamisho huo kwa miezi kadhaa, lakini ni wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia ambapo mchezaji huyo na Inter Miami alifikia makubaliano ya mwisho na kutatua suala la haki za usajili zilizokuwa zikishikiliwa na timu ya LA Galaxy. Inter Miami na LA Galaxy zote zinashiriki Ligi Kuu Marekani (MLS).
MIAMI, MAREKANI: KIUNGO wa kimataifa wa Brazil, Carlos Henrique Casimiro maarufu Casemiro anatarajiwa kujiunga na Inter Miami ambayo mmoja wa wamiliki wake ni staa wa zamani wa England na Manchester United, David Beckham.
Kwa mujibu wa mwandishi maarufu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano kupitia akaunti yake ya X, Casemiro alikuwa karibu kukamilisha uhamisho huo kwa miezi kadhaa, lakini ni wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia ambapo mchezaji huyo na Inter Miami alifikia makubaliano ya mwisho na kutatua suala la haki za usajili zilizokuwa zikishikiliwa na timu ya LA Galaxy. Inter Miami na LA Galaxy zote zinashiriki Ligi Kuu Marekani (MLS).
Inadaiwa kuwa shauku ya Casemiro kucheza pamoja na Lionel Messi ilichangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha dili hilo, licha ya changamoto za kisheria zilizokuwepo kutokana na LA Galaxy kuwa na haki za kipaumbele iwapo mchezaji huyo angehamia MLS. Na sasa Inter Miami inatarajiwa kuimarisha safu yake ya kiungo kwa kuwa na nyota huyo mwenye uzoefu mkubwa.
Ushindani uliokuwepo kati ya Casemiro na Messi katika miaka yao wakati wakicheza Real Madrid na Barcelona mtawalia, utawekwa kando wakijiandaa kushirikiana katika timu moja ili kuiwezesha kutisha msimu ujao wa mashindano ya soka Marekani na Amerika Kaskazini.
Kutoka kwenye mechi kali za El Clasico wakati wakiwa Hispania hadi kushirikiana chumba kimoja cha kubadilishia nguo na malengo ya pamoja ndani ya kikosi cha Inter Miami, Casemiro na Messi sasa watakuwa upande mmoja.
Casemiro anatarajiwa kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya Inter Miami msimu ujao pamoja na Antoine Griezmann, staa wa zamani wa Atletico Madrid na huenda pia Robert Lewandowski ikiwa usajili wake utakamilika. Iwapo usajili huo utathibitishwa, utaongeza idadi ya mastaa wa kimataifa wanaocheza MLS, kufuatia uwepo wa Messi, Son Heung-min, Thomas Muller, Marco Reus na Griezmann.