Bayern Munich yatuliza mashabiki majeraha ya Kane
Muktasari:
- Kane alikosa mechi ya Bundesliga dhidi ya Freiburg pamoja na mchezo wa kirafiki wa timu ya taifa ya England dhidi ya Japan kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu aliyoyapata ghafla.
MUNICH, UJERUMANI: BAYERN Munich imetoa taarifa njema kuhusu mshambuliaji wao tegemeo, Harry Kane, huenda akarejea uwanjani mapema kabla ya mechi muhimu dhidi ya Real Madrid katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inayopigwa kesho usiku.
Kane alikosa mechi ya Bundesliga dhidi ya Freiburg pamoja na mchezo wa kirafiki wa timu ya taifa ya England dhidi ya Japan kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu aliyoyapata ghafla.
Kocha wa England, Thomas Tuchel amesema jeraha hilo si kubwa na linaweza kupona haraka. “Ni jeraha dogo lililotokea ghafla,” amesema.
Mjumbe wa bodi ya Bayern anayeshughulikia michezo, Max Eberl amesema madaktari wanaendelea kumhudumia Kane na wana matumaini atakuwa fiti kwa mchezo dhidi ya Madrid.
Kocha wa Bayern, Vincent Kompany alionyesha matumaini makubwa, akisema hali inaonyesha Kane ataweza kucheza.
Mshambuliaji huyo tayari amefunga mabao 48 katika michuano yote msimu huu na ana mabao 31 Bundesliga, akiwa katika harakati za kuvunja rekodi ya Robert Lewandowski ya mabao 41 kwa msimu mmoja.
Kurejea kwake kutakuwa pigo kubwa kwa Real Madrid, huku Bayern wakilenga kuandika historia mpya ya mabao mengi katika msimu mmoja wa Bundesliga.