Barcelona ‘yajilipua’ kwa Harry Kane
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya kuonyesha nia yao ya kumsajili, mabingwa hao wa Catalonia wamekubaliana kusubiri hadi baada ya Kane kumaliza majukumu yake katika Kombe la Dunia, ndipo watakapopitia upya hali ya uhamisho huo.
LONDON, ENGLAND: BARCELONA wamewasiliana na wawakilishi wa Harry Kane ili kuchunguza uwezekano wa kumsajili nahodha huyo wa England.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya kuonyesha nia yao ya kumsajili, mabingwa hao wa Catalonia wamekubaliana kusubiri hadi baada ya Kane kumaliza majukumu yake katika Kombe la Dunia, ndipo watakapopitia upya hali ya uhamisho huo.
Mshambuliaji huyo wa Bayern Munich, mwenye umri wa miaka 32, amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake, na Barcelona wanatafuta njia za kifedha zitakazowawezesha kukamilisha usajili huo mkubwa.
Hata hivyo, Kane ana furaha kubwa kuendelea kuichezea Bayern Munich, na mabingwa hao wa Bundesliga hawana nia ya kumuachia mshambuliaji wao tegemeo.
Inaelezwa pia kuwa baada ya simu kutoka Barcelona ya kuulizia uwezekano wa uhamisho, kambi ya Kane ilikataa kuendeleza mazungumzo hayo. Badala yake, lengo lao baada ya Kombe la Dunia ni kuanza mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya na Bayern Munich.
Kwa sasa, hali halisi ya suala hilo itajulikana baada ya England kumaliza kampeni yao ya Kombe la Dunia, kwani Kane ameweka akili yake yote katika mashindano hayo. England itacheza dhidi ya DR Congo katika hatua ya 16 Bora mjini Atlanta kesho Jumatano.
Kane tayari amefunga mabao matatu katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia, akifuatia msimu bora akiwa Bayern ambapo alifunga mabao 61 katika mechi 51.
Barcelona wanatafuta mshambuliaji mpya baada ya kuondoka kwa Robert Lewandowski.
Vyanzo vinaeleza kuwa iwapo kutakuwa na dalili yoyote kwamba uhamisho huo unaweza kufanikiwa, Barcelona wako tayari kufanya kila wawezalo ili kuhakikisha wanamnasa Harry Kane.