Barcelona kuuza, kununua straika
Muktasari:
- Vyanzo mbalimbali vilivyozungumza na ESPN vimedai kwamba hadi washambuliaji wawili wapya wanaweza kujiunga na Barca, huku Torres akiwa mchezaji mkubwa kikosini anayeweza kuondolewa ili kuimarisha safu ya ushambuliaji.
BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA inapanga kufanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya ushambuliaji katika dirisha lijalo la usajili la majira ya kiangazi, mpango unaohusisha kusikiliza ofa kwa ajili ya kumuuza straika Ferran Torres ili kufanikisha usajili wa wachezaji wapya.
Vyanzo mbalimbali vilivyozungumza na ESPN vimedai kwamba hadi washambuliaji wawili wapya wanaweza kujiunga na Barca, huku Torres akiwa mchezaji mkubwa kikosini anayeweza kuondolewa ili kuimarisha safu ya ushambuliaji.
Kwa lengo la kuongeza mapato na kuwekeza katika usajili mpya, klabu inapendelea kumuuza Torres mwenye umri wa miaka 26 ambaye mkataba wake unamalizika 2027.
Kwa sasa, jina lake linaonekana kuwa kipaumbele zaidi kuondoka kuliko mkongwe Robert Lewandowski, licha ya tofauti kubwa ya umri kati yao, ambapo mpango wa Barcelona kwa mshambuliaji huyo ni kumuongezea mkataba ambao unatarajiwa kuisha mmwishi wa msimu huu.
Mkurugenzi wa michezo wa Barca, Deco de Souza ndiye anayesimamia mchakato wa kutafuta mbadala wa Torres na miongoni mwa majina yanayozungumzwa ni mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez.
Wakati huohuo, Barcelona pia inatafuta njia za kuendelea kubaki na Marcus Rashford, ambaye amekuwa mchezaji muhimu kwa timu, huku klabu ikiwa na chaguo la kumnunua moja kwa moja mchezaji huyo wa kimataifa wa England kutoka Manchester United kwa Euro 30 milioni, ingawa inapendelea kupunguziwa bei au kuongeza muda wa mkopo wake kwa msimu mmoja zaidi.
Hata hivyo, Barcelona inatambua kuwa mipango yote hiyo ama kumuongezea mkataba Lewandowski, kumsajili Alvarez na kumbakiza Rashford ni suala linalohitaji makubaliano na ndiyo maana wanaendelea kuchambua chaguo mbadala ili kuimarisha nafasi ya mshambuliaji wa kati pamoja na nafasi za pembeni.