Barca mambo magumu dili la Marcus Rashford
Muktasari:
- Katika makubaliano ya mkataba wa mkopo, Man United iliweka kipengele kilichokuwa kinaitaka Barca kulipa Pauni 26 milioni ili kumsajili mazima Rashford ikiwa itaridhishwa na kiwango chake.
BARCELONA italazimika kuanza upya mazungumzo na Manchester United ikiwa inahitaji kumsainisha mkataba wa moja kwa moja Marcus Rashford, baada ya ripoti za ndani kufichua kuwa kipengele kilichokuwa kinawawezesha kumsajili kwa Pauni 26 milioni kimekwisha muda wake mwezi uliopita.
Hali hiyo imeliingiza dili hilo katika wakati mgumu, kwani Barca inahofia huenda Man United ikataja bei kubwa zaidi ya ile iliyokuwepo hapo awali.
Rashford, ambaye msimu huu anacheza kwa mkopo Barcelona, ameonyesha kiwango bora sana kiasi cha kuivutia timu hiyo kutaka kumsajili mazima, lakini changamoto kubwa ilikuwa ni ada ya uhamisho.
Katika makubaliano ya mkataba wa mkopo, Man United iliweka kipengele kilichokuwa kinaitaka Barca kulipa Pauni 26 milioni ili kumsajili mazima Rashford ikiwa itaridhishwa na kiwango chake.
Hata hivyo, baada ya kuamua kumsajili mazima, Barca ilikuwa ikiomba kupunguziwa bei, jambo ambalo Man United ililikataa, na taarifa zinadai kuna timu ipo tayari kulipa Pauni 50 milioni ili kumpata mchezaji huyo.
Rashford mwenyewe ameonyesha nia ya kutaka kuendelea kusalia Barca, lakini hawezi kufanya chochote kwa sababu bado ana mkataba unaomalizika 2028.
John Stones
BEKI wa Manchester City na timu ya taifa ya England, John Stones, 31, hatarajiwi kupewa mkataba mpya na Manchester City katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Hali hiyo imezifanya timu kadhaa kuanza kufuatilia uwezekano wa kumsajili, ikiwemo klabu yake ya zamani, Everton, ambayo inaonyesha nia ya kuhitaji huduma yake tangu mwaka jana.
Mkataba wa sasa wa Stones unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu. Moja ya sababu inayodaiwa kuwafanya Man City wasimpe mkataba mpya ni majeraha ya mara kwa mara ambayo amekuwa akiyapata.
Sandro Tonali
WAKALA wa kiungo wa Newcastle United, Sandro Tonali, 25, wamewasiliana na Real Madrid ikiwa ni katika harakati za kutafuta klabu mpya kwa mchezaji huyo.
Mbali na Real Madrid, Manchester City pia inaonyesha nia ya kumsajili Tonali, ambaye hatokuwepo katika Kombe la Dunia baada ya Italia kushindwa kufuzu.
Tonali anaonekana kuwa ni mmoja kati ya wachezaji watakaokuwa na ushindani mkubwa sokoni, ambapo timu nyingi zinahitaji huduma yake.
Bernardo Silva
BARCELONA inaongoza mbio za kumsajili kiungo wa Ureno, Bernardo Silva, 31, kutoka Manchester City, ambaye atapatikana kwa uhamisho wa bure katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Inaelezwa kuwa Silva yupo tayari kuondoka Man City mkataba wake utakapomalizika, jambo linalowapa Barcelona nafasi nzuri ya kumnasa bila kulipa ada ya usajili.
Iwapo dili hilo litakamilika, Barcelona itakuwa imepata kiungo mwenye uzoefu mkubwa, ingawa baadhi ya ripoti zinadai staa huyo ana ofa kubwa kutoka Saudi Arabia.
Christian Kofane
ARSENAL inaendelea kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji kijana wa kimataifa wa Cameroon, Christian Kofane, 19, anayekipiga katika kikosi cha Bayer 04 Leverkusen.
Inaelezwa kuwa Leverkusen inahitaji hadi Pauni 60 milioni ili kumuuza mchezaji huyo katika dirisha la majira ya kiangazi.
Kofane kwa sasa ni mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Leverkusen, na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029.
Jules Kounde
MANCHESTER City, Liverpool, na Chelsea zinafuatilia kwa karibu hali ya beki wa kimataifa wa Ufaransa, Jules Kounde, 27, anayekipiga katika kikosi cha Barcelona.
Kounde anawindwa na vigogo hao kutokana na kiwango chake na uwezo mkubwa wa kucheza nafasi mbalimbali katika safu ya ulinzi.
Iwapo Barcelona itakuwa tayari kusikiliza ofa, ushindani wa kumpata unaweza kuwa mkali kati ya vigogo hao wa England, ambao wapo katika mazungumzo pia na wakala wake.
Denzel Dumfries
BEKI wa kulia wa kimataifa wa Uholanzi, Denzel Dumfries, 29, anayekipiga katika klabu ya Inter Milan, amewekwa sokoni.
Tayari klabu kadhaa kutoka England zimeulizia kuhusu upatikanaji wake, ikiwemo Liverpool, Manchester City, Manchester United, Chelsea, Tottenham Hotspur, na Newcastle United.
Hata hivyo, licha ya Inter kuwa tayari kumujuza suala la kuipata saini yake, halionekani kuwa jepesi kutokana na utitiri wa timu zinazomtaka staa huyo.
Manuel Locatelli
KOCHA mpya wa Tottenham, Roberto De Zerbi, anatajwa kuwa na nia ya kumsajili kiungo wa Juventus na timu ya taifa ya Italia, Manuel Locatelli, 28, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
De Zerbi anaamini Locatelli anaweza kuwa nyongeza muhimu katika mfumo wake wa uchezaji, hivyo ameshamjumuisha katika orodha ya mastaa anaowahitaji.
Kwa sasa kocha huyo anapambana kuhakikisha Spurs inasogea nafasi za juu kidogo kutoka ilipo sasa, ambapo ikiendelea kupata matokeo mabaya inaweza kujikuta ikishuka daraja.
Yan Diomande
MANCHESTER United na Liverpool zinapigana vikumbo kuiwania saini ya winga wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yan Diomande, 19.
Diomande anaonekana kuwa miongoni mwa mastaa wanaokuja kwa kasi, na timu hizo mbili zimekuwa zikimfuatilia kwa muda sasa na zinaona ni wakati sahihi kuwasilisha ofa katika dirisha lijalo.
Mkataba wa sasa wa Diomande unatarajiwa kumalizika 2030, na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 29 za michuano yote na kufunga mabao 11.