Arteta, Slot vita nje ndani yani
Muktasari:
- Miamba hiyo imekuwa ikipigana vipushi kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England kwa muda mrefu msimu huu na inaweza kupigana vikumbo pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL na Liverpool zinaweza kujikuta kwenye wiki moja matata itakayowafanya kuwa kwenye vita kali ya kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England na ule wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Miamba hiyo imekuwa ikipigana vipushi kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England kwa muda mrefu msimu huu na inaweza kupigana vikumbo pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Arsenal na Liverpool kama zitaibuka na ushindi katika raundi mbili zijazo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, basi zinaweza kukutana kwenye nusu fainali.
Mechi ya kwanza ya nusu fainali itafanyika Aprili 29/30, huku ile ya marudiano itafanyika wiki inayofuatia.
Hiyo ina maana, timu moja inaweza kuishinda nyingine na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya siku chache kabola hazijakutana tena kwenye mchezo muhimu kabisa wa Ligi Kuu England.
Arsenal itakwenda Anfield kumenyana na Liverpool, Mei 10 katika mechi ambayo huenda ikatoa taswira kamili ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Arsenal ilitarajia kumenyana na West Ham United jana Jumamosi na ushindi utawafanya kupunguza pengo la pointi na kubaki tano, huku Liverpool ikiwa na kibarua mbele ya Manchester City, leo Jumapili,
Kama Liverpool itashinda, kisha Arsenal ikishinda mechi yake moja ya mkononi itafanya pengo kuwa pointi tano. Lakini, sare au kichapo kwa Liverpool, kisha Arsenal ikashinda kiporo chake, endapo itakuwa imeshinda jana, basi pengo la pointi litakuwa limepungua zaidi kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.