Arteta, karata ya mwisho mkononi wikiendi hii

Saturday September 11 2021
EDO PIC
By Edo Kumwembe

MIKEL Arteta ni mmoja kati ya makocha wenye bahati duniani. Amefungwa mechi tatu za kwanza za Ligi Kuu ya England na inaonekana kama vile waajiri wake hawana wasiwasi naye. Inashangaza sana hasa katika maisha ya kileo.
Katika hizo mechi imeonekana wazi kwamba kazi yake haiwezi. Amefungwa na timu moja nyepesi, Brentford halafu akafungwa na timu mbili ngumu, Manchester City na Chelsea. Walau angeshinda mechi ya kwanza halafu akafungwa hizi mbili.
Wikiendi hii timu yake itakuwa inacheza na Norwich. Pamoja na uvumilivu mkubwa wa watu wa Arsenal juu yake nadhani hii inaweza kuwa mechi yake ya mwisho Emirates. Kuna kujidanganya kwingi pale Emirates. Nataka kujua kama watamvumilia.
Inadaiwa kwamba wakubwa wa Arsenal wanaamini kwamba Arteta ni kocha wa mipango mirefu. Wanaamini amekusanya wachezaji wengi vijana anaowataka na sasa ni wakati wa kuanza kazi. Wanaamini kwamba mechi hizi tatu zimeharibika kwa sababu alikuwa na wachezaji wengi majeruhi.
Bahati nzuri kwake ni kwamba wale wachezaji wenye majeruhi wamerudi na Arsenal inacheza na timu kama Norwich. Atakuwa na kisingizio gani tena endapo Arsenal itafungwa au kutoka sare wikiendi hii? mabosi wake wataendelea kuamini katika mchakato?
Hayo yote yanatokea wakati mtu kama Antonio Conte akiwa hana kazi. Haya yanatokea wakati mpaka sasa inaonekana Arteta yupo nyuma kitaalamu kwa baadhi ya makocha wanaofundisha timu za kawaida kama vile, Brendan Rodgers anayefundisha Leicester City na ameigeuza timu hiyo kuwa tishio.

Advertisement