Arsenal yamaliza EPL kibabe, West Ham yashuka daraja
Muktasari:
- Arsenal imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) baada ya kukaa bila taji hilo kwa miaka 22.
LONDON, ENGLAND: Arsenal imenogesha sherehe zake za ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) msimu huu baada ya leo Jumapili, Mei 24, 2026 kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Crystal Palace kwenye Uwanja wa Selhurst Park, London.
Mabao ya Arsenal ambayo leo inakabidhiwa taji la EPL, yamefungwa na Gabriel Jesus na Noni Madueke huku la Palace likipachikwa na Jean-Phillipe Mateta.
Licha ya Mikel Arteta kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi na kupumzisha wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza, Arsenal imeonyesha kiwango bora katika mchezo huo.
Katika Uwanja wa Etihad, wenyeji Man City wamemuaga vibaya meneja wao, Pep Guardiola baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Aston Villa.
Imekuwa siku ya huzuni na simanzi kwa West Ham United ambayo licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Leeds United, imeshuka rasmi daraja.
West Ham imejikuta ikimaliza katika nafasi ya 18 ikiwa na pointi 39 hivyo kuungana na Burnley na Wolves ambazo zilishatangulia kuangukia Championship.
West Ham ingeweza kubakia iwapo Tottenham Hotspur ingepoteza mchezo wake wa nyumbani dhidi ya Everton.
Hata hivyo Spurs imepata ushindi wa bao 1-0 ambao umeifanya imalize katika nafasi ya 17 na pointi 41.
Timu za Arsenal, Man City, Man United, Liverpool na Aston Villa zimefanikiwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Bournemouth na Sunderland zimefuzu kucheza Europa League msimu ujao huku Brighton ikifuzu kuingia raundi ya awali ya mchujo ya UEFA Conference League.
MATOKEO YA EPL LEO
Crystal Palace 1-2 Arsenal
Man City 1-2 Man City
West Ham 3-0 Leeds United
Tottenham Hotspur 1-0 Everton
Fulham 2-0 Newcastle United
Liverpool 1-1 Brentford
Nottingham Forest 1-1 Bournemouth
Sunderland 2-1 Chelsea
Brighton 0-3 Man United
Burnley 1-1 Wolves