Arsenal ngoma ngumu

Muktasari:

  • Arsenal kijasho kinawatoka baada ya kutambua ratiba yao ni ngumu sana kabla ya kwenda kuwakabili mahasimu wao Tottenham Hotspur kwenye North London Derby.

LONDON,ENGLAND: Arsenal kijasho kinawatoka baada ya kutambua ratiba yao ni ngumu sana kabla ya kwenda kuwakabili mahasimu wao Tottenham Hotspur kwenye North London Derby.


Arsenal bado inafukuzia mataji Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mwezi ujao utakuwa muhimu kwelikweli kwenye kutambua matumaini yao ya kufanya vizuri kwenye michuano yote wanayoshindania ubingwa.


Wakati Spurs yenyewe ikielekeza nguvu kwenye michuano ya Ligi Kuu England pekee, wakisaka tiketi ya kuwamo kwenye Top Four ili kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, wakitambua vita yake dhidi ya Aston Villa na Manchester United.


Kipute cha North London Derby kitapigwa Aprili 28. Mechi ya mwisho ya kikosi cha Spurs chini ya Kocha Ange Postecoglou itacheza kabla ya kuwakabili Arsenal ni ule mchezo wa ugenini kuwakabili Newcastle United, Aprili 13, hiyo ina maana itakuwa na siku 15 za kujiandaa na mechi hiyo dhidi ya jeshi la Mikel Arteta.


Wakati kwa upande wa Arsenal kwa siku hizo 15 ambazo Spurs itakuwa mapumziko, wenyewe watakuwa na mechi nne na itakipiga na Aston Villa (Aprili 14), Wolves (Aprili 20) na Chelsea (Aprili 23) kwenye ligi na Bayern kwenye Mabingwa Ulaya.


Mechi hiyo ya marudiano na Bayern itafanyika Aprili 17, itakuwa ugenini Allianz Arena huko Ujerumani.


Ratiba ya awali ilikuwa ikionyesha Spurs na Man City zilipangwa kufanyika kwenye wikiendi ya Aprili 20 na 21, lakini kitendo cha miamba hiyo ya Pep Guardiola kusonga mbele kwenye Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya kimefanya mechi hiyo iahirishwe na bado haijapangiwa siku.