Arsenal kuivaa Bournemouth mchana leo ikisaka rekodi

Muktasari:

  • Kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta tayari kimeshashinda mechi 25 msimu huu, huku kikitoka sare mara tano na kupoteza tano, kikijinafasi kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.

LONDON, ENGLAND. Arsenal huenda ikafikia rekodi yake tamu ya ushindi wa mechi kibao kwenye Ligi Kuu England wakati itakapokipiga na Bournemouth uwanjani Emirates mchana wa leo Jumamosi.

Kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta tayari kimeshashinda mechi 25 msimu huu, huku kikitoka sare mara tano na kupoteza tano, kikijinafasi kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo.

Arsenal imeweka pengo la pointi tano dhidi ya Liverpool kwenye mchakamchaka wa kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na mjadala huo unaweza kufungwa kabisa wikiendi hii endapo kama Jurgen Klopp na kikosi chake atapoteza mbele ya Tottenham Hotspur na kisha Arteta akawachapa Cherries.

The Gunners pia wapo juu kwa pointi moja dhidi ya Manchester City, ambapo zinaweza kuongezeka na kuwa pointi nne endapo wataichapa Bournemouth, lakini mabingwa hao watetezi bado wana mchezo mmoja mkononi, hivyo mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu zipo mikononi mwao.

Ushindi wa Arsenal unaweza kuzidisha presha Man City, kabla ya kukipiga na Wolves baadaye, huku chama hilo la Arteta kama litapata ushindi, basi utakuwa ni ushindi wa 26 na kufikia rekodi zao za juu kabisa walizowahi kuzifikia huko nyuma kwenye Ligi Kuu England.

Arsenal ilifikia ushindi wa mechi 26 za ligi mara tatu tu kwenye misimu iliyopita, ilikuwa msimu wa 2001-02 na 2003-04, ambao hawakupoteza hata mchezo mmoja, huku msimu mwingine ni wa 2022-23, Arsenal ilikaa kileleni kwa siku 248 kabla ya kutibua mambo dakika za mwisho na Man City kubeba ubingwa.

Wakati Arsenal ikifukuzia rekodi hiyo ya ushindi, imebakiza mabao manne pia kuvunja rekodi yao nyingine ya juu kwenye Ligi Kuu England kwa msimu mmoja, baada ya sasa kuwa imeshafunga mabao 85.

Arsenal ilifunga mabao 88 katika msimu wa 2022-23, wakati timu hiyo ilipokuwa chini ya Arsene Wenger na katika msimu wa 2004-05 ilifunga mabao 87.