Arsenal kuhamia Wembley kupisha maboresho Uwanja wa Emirates
Muktasari:
- Arsenal kwa sasa, inautumia uwanja wa Emirates kwa mechi zake za nyumbani, lakini uongozi wa timu hiyo umepanga kuupanua uwanja huo unaochukua mashabiki 60,700 walioketi na kuufanya kuingiza mashabiki 70,000.
KLABU ya Arsenal huenda ikahamishia mechi zake zotw kwenye Uwanja wa Wembley, ili kupisha maboresho ya Uwanja wa Emirates, kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka kwa The Telegraph.
Arsenal kwa sasa, inautumia uwanja wa Emirates kwa mechi zake za nyumbani, lakini uongozi wa timu hiyo umepanga kuupanua uwanja huo unaochukua mashabiki 60,700 walioketi na kuufanya kuingiza mashabiki 70,000.
Mpango huo umechukua nafasi kubwa katika vikao vya uongozi wa klabu hiyo ya Kaskazini mwa London, ambao umedhamiria kupunguza msongamano wa kusubiri tiketi za msimu, ambapo zaidi ya mashabiki 100,000 wako katika orodha hiyo na inakadiriwa itachukua hadi miaka 20 kuitoa yote.
Uwanja wa Emirates uliojengwa kwa Pauni 390 milioni na kufunguliwa mwaka 2006 ndio ulikuwa mkubwa zaidi jijini London kwa wakati huo, lakini ndani ya muongo mmoja uliopita, Arsenal wamepoteza nafasi hiyo kwa West Ham United na wapinzani wao wakubwa Tottenham Hotspur.
West Ham walihamia kwenye Uwanja wa London (London Stadium) mwaka 2016, unaochukua mashabiki 62,500.
Tottenham walimaliza ujenzi wa uwanja wao mpya mwaka 2019, unaochukua mashabiki 62,850 na kwa sasa ni mkubwa zaidi kwa klabu zote jijini London.
Arsenal waliwahi kucheza mechi zote za Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Wembley kati ya 1998 na 2000. Wakiwa na wachezaji kama Thierry Henry, Dennis Bergkamp na Patrick Vieira na waliweza kuvutia mashabiki zaidi ya 71,000 katika michezo sita, lakini walishinda mechi mbili pekee, wakatoka sare mara moja na kupoteza mechi tatu.
Kwa ujumla, Arsenal imecheza mechi 59 kwenye Uwanja wa Wembley, ikishinda 32, sare 8 na kupoteza 20.
Iwapo upanuzi mkubwa utaendelea, Arsenal itahitaji kutafuta uwanja mbadala kwa mechi za nyumbani na Wembley unaonekana kuwa chaguo kuu. Hii itafuata nyayo za Tottenham waliolipa Pauni 15 milioni kucheza mechi zao kwenye uwanja huo kwa karibu miaka miwili walipokuwa wakimalizia ujenzi wa uwanja mpya.
Mipango ya Arsenal pia imepata msukumo wa upanuzi wa uwanja huo, baada ya Santiago Bernabeu wa Real Madrid, uliofanyiwa maboresho kati ya mwaka 2019 hadi 2024, ukiwa wa kisasa na wenye matumizi mengi ya kidijitali.
Gharama ya mradi huo zinakadiriwa kufikia Pauni 500 milioni, lakini klabu bado haijafikia hatua ya kuomba kibali rasmi cha ujenzi.
Arsenal wanaelewa changamoto za kisheria na za mipango mji kutoka halmashauri ya Islington, ingawa hapo awali halmashauri hiyo ilikubali maendeleo yaliyozidi kikomo cha mita 30.
Kwa msimu wa 2023/24, Arsenal ilipata Pauni 131.7 milioni kutokana na mapato ya siku ya mechi, ambapo Pauni 105.2 milioni yalitokana na mapato ya milangoni kwa wastani wa miaka mitatu kuanzia 2021 hadi 2024.
Hii ni takriban Pauni 19 milioni pungufu ya Manchester United na Pauni 6 milioni chini ya Tottenham, kwa mujibu wa takwimu za Deloitte.