Aondoke Salah, aje Osimhen

Muktasari:

  •  
  • Mo Salah, amekuwa mchezaji muhimu huko Anfield tangu alipotua mwaka 2017, lakini sasa anahusishwa na mpango wa kutaka kuachana na timu hiyo, huku Kocha Jurgen Klopp akiachana na miamba hiyo mwisho wa msimu.

LIVERPOOL, ENGLAND: Staa wa Liverpool, Steve Nicol anaamini straika Victor Osimhen utakuwa usajili mzuri sana kwa miamba hiyo ya Anfield wakati alipojaribu kujibu swali anadhani ni nani atafaa zaidi kurithi buti za Mohamed Salah.


Mo Salah, amekuwa mchezaji muhimu huko Anfield tangu alipotua mwaka 2017, lakini sasa anahusishwa na mpango wa kutaka kuachana na timu hiyo, huku Kocha Jurgen Klopp akiachana na miamba hiyo mwisho wa msimu.


Liverpool iligoma kumuuza Mo Salah kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana wakati klabu za Saudi Arabia zilipoonyesha dhamira ya kunasa saini yake, lakini kinachoelezwa timu hizo zitarudi mwisho wa msimu kuulizia upatikanaji wa huduma ya supastaa huyo wa kimataifa wa Misri.


Kuondoka kwa Mo Salah bila shaka kutaacha pengo kubwa Liverpool kutokana na uwezo wa kufunga mabao wa mchezaji huyo na sasa Nicol anaamini timu hiyo inapaswa kuleta mtu mwingine mwenye uwezo wa kufunga.


Alisema: “Ukweli ni kwamba Mo Salah anaondoka, inaweza kuwa mwaka huu au mwakani. Osimhen? Nadhani utakuwa usajili mzuri Liverpool. Kwenye kiungo kuna watu mahiri kama usajili wa Alexis Mac Allister na Dominik Szoboszlai, Endo naye ameonyesha ubora mkubwa.”


Nicol alidai kumchukua Osimhen, ambaye aliisaidia Napoli kushinda ubingwa wa Serie A, kutamfanya Darwin Nunez abadilishiwe nafasi na kucheza pembeni. Staa huyo wa zamani wa Benfica, Nunez ameonyesha soka zuri, lakini ubora wake wa kutumbukiza mipira nyavuni hauwezi kumfikia Osimhen, ambaye anakuwa hatari mbele ya goli.


Osimhen, ambaye ni Mnigeria alinaswa na Napoli akitokea Lille msimu kadhaa iliyopita, siku za karibuni alihusishwa sana na Chelsea, inayodaiwa kusaka straika wa kuwapigia mabao.