Antony kumpisha Olise Manchester United

Muktasari:

  • Antony amekuwa kwenye orodha hiyo kwa sababu hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa tangu atue Man United mwaka 2022 kwa ada ya uhamisho wa Euro 95 milioni.

MABOSI wa Manchester United wanasubiria ofa kwa ajili ya kumuuza winga wao raia wa Brazil, Antony, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ajili ya kupata pesa itakazotumia kufanya usajili wa kiungo wa Crystal Palace na Ufaransa, Michael Olise, 22 ambaye pia anawindwa na Manchester City.

Antony amekuwa kwenye orodha hiyo kwa sababu hajaonyesha kiwango kilichotarajiwa tangu atue Man United mwaka 2022 kwa ada ya uhamisho wa Euro 95 milioni.

Msimu huu amecheza mechi 36 za michuano yote, akafunga mabao matatu na kutoa asisti mbili pekee.

Palace ipo tayari kumuuza Olise lakini ada yake ya uhamisho inaweza kufikia Pauni 70 milioni kutokana na kiwango chake na urefu wa mkataba wake unaomalizika mwaka 2027.

Hata hivyo, mwezi uliopita wakala wa mshambuliaji huyu alisema bado hawajafikiria kuondoka licha ya tetesi zinazodai hivyo.

Antony bado ana mkataba wa kuitumikia Man United hadi mwaka 2027.