Ancelotti: Neymar kurejea wiki ijayo
Muktasari:
- Hata hivyo, kabla ya mchezo huo, kocha Carlo Ancelotti alimzungumzia mchezaji huyo anayesumbuliwa na jeraha, akisema amekuwa akiendelea vyema kupona na kwamba anatarajiwa kurejea kwenye mazoezi kamili ya timu wiki ijayo.
NEW JERSEY, MAREKANI: JANA, Jumamosi usiku, Brazil ilikuwa uwanjani MetLife huko New Jersey kukabiliana na Morocco katika mechi ya kundi C la Kombe la Dunia 2026, lakini nyuma ya mchezo huo mashabiki walikuwa wakijiuliza juu ya mustakabali wa supastaa wa nchi hiyo, Neymar Jr.
Hata hivyo, kabla ya mchezo huo, kocha Carlo Ancelotti alimzungumzia mchezaji huyo anayesumbuliwa na jeraha, akisema amekuwa akiendelea vyema kupona na kwamba anatarajiwa kurejea kwenye mazoezi kamili ya timu wiki ijayo.
Kutokana na hilo, hali hiyo inaweza kumpa nafasi ya kupata dakika chache za kucheza dhidi ya Haiti katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi utakaochezwa Ijumaa, Juni 19.
Ancelotti alisema: “Neymar anafanya kazi kwa bidii kubwa ili kupona haraka iwezekanavyo. Tunatarajia atapona na kurejea kujiunga na kikosi wiki ijayo. Tunapomuita Neymar, hatumuiti tu kwa sababu ya uwezo wake wa kiufundi ambao hauna shaka, bali pia kwa uzoefu wake na mfano anaoweza kutoa kwa wachezaji vijana waliopo kwenye kundi hili.”
Hata hivyo, Ancelotti na benchi lake la ufundi wanaweza kuamua kutoharakisha kurejea kwa Neymar, kwani kwa kujiunga na kikosi wiki ijayo, muda wa kuwa tayari kwa mchezo dhidi ya Haiti unaweza kuwa mfupi.
Kutokana na hali hiyo, mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Scotland inaweza kuwa bora zaidi kwa Neymar kurejea uwanjani.