Amorim: Mastaa Man United walaumiwe
Muktasari:
- Tajiri mpya wa mashetani hao wekundu, Sir Jim Ratcliffe, hivi karibuni aliripotiwa anapanga kuondoa wafanyakazi zaidi ya 200 katika hatua ya kupunguza gharama za matumizi.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amesema wachezaji wa Manchester United ndio wanapaswa kulaumiwa na kuwajibika kwa hali inayoendelea ya kufukuzwa kwa wafanyakazi wa timu hiyo.
Tajiri mpya wa mashetani hao wekundu, Sir Jim Ratcliffe, hivi karibuni aliripotiwa anapanga kuondoa wafanyakazi zaidi ya 200 katika hatua ya kupunguza gharama za matumizi.
Mbali ya kufukuza wafanyakazi, Ratcliffe pia amepandisha bei za viingilio kwenye mechi mbalimbali.
Amorim anaamini ikiwa timu hiyo ingekuwa na matokeo mazuri uwanjani huenda ajira za watu walioondoshwa na wanaotarajiwa kuondoshwa zingekuwepo hadi sasa.
“Timu yetu kwa muda mrefu haijafanya vizuri. Tunawanunua wachezaji, tunatumia pesa, kisha hatupati matokeo. Hivyo, matatizo haya ni yetu. Watu wanapoteza kazi zao hivyo lazima tukubali hilo.
“Shida kubwa ni viwango vya wachezaji, hatuko kwenye Ligi ya Mabingwa, hivyo mapato pia yamepungua, kila mtu hapa anajua ni namna gani huwa ngumu kwa watu wanaopoteza kazi zao. Tunajua hilo ni kosa letu sisi tunaofundisha na kucheza ndio tunaohusika na hilo. Ni muhimu sana kutolipuuzilia mbali jambo hili, hivyo njia pekee ya kusaidia ni kushinda mechi, kwenda Ligi ya Mabingwa Ulaya.”
Katika majira ya kiangazi mwaka jana wafanyakazi 250 wa timu hiyo walivunjiwa mikataba, pia bei za tiketi zilipandishwa na punguzo kwa watoto na wastaafu ziliondolewa.
Kocha mstaafu Sir Alex Ferguson naye alifutwa kazi kama balozi, huku mkuu wa shughuli za timu, Jackie Kay ambaye anahusudiwa kuwa kama “mama” kwa wachezaji pia yupo hatarini kupoteza kazi yake.