Amorim atabasamu ishu ya Donnarumma
Muktasari:
- Man United imekuwa na shughuli nyingi dirisha hili la usajili la kiangazi na imekamilisha usajili wa wachezaji wakubwa kama Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim aliachia tabasamu zito alipoulizwa na shabiki mmoja kama atamsajili nyota wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma.
Man United imekuwa na shughuli nyingi dirisha hili la usajili la kiangazi na imekamilisha usajili wa wachezaji wakubwa kama Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko.
Hata hivyo, kusajili kiungo mpya ndiyo inaonekana kipaumbele cha Man United kwa sasa na staa wa Brighton, Carlos Baleba ndiye anayetajwa.
kiwango cha chini cha Andre Onana miaka miwili iliyopita, kimedaiwa kutoridhisha benchi la ufundi ambalo ripoti zinadai linafikiria kumsajili kipa mwingine.
Tetesi za Man United kuwa katika mpango wa kumsajili Donnarumma, 26, zimepamba moto wiki iliyopita hususan baada ya PSG kumsajili kipa Lucas Chevalier kutoka Lille, hivyo kufungua milango kwa kipa huyo kuondoka.
Amorim, 40, aliulizwa kuhusu uvumi huo na shabiki mmoja nje ya Old Trafford alipokuwa akisaini jezi na skafu.
“Hey Ruben, tunamsajili nani? Je, tumempata Donnarumma?”
Amorim alijibu: “Samahani?”
Shabiki alimjibu tena: “Je, tumempata Donnarumma?”
Licha ya swali hilo, Amorim hakujibu na alibaki mpole kisha akatabasamu kidogo na kuendelea kusaini vile alivyopewa kusaini.
Hata hivyo, mpango wa kusajili kipa mpya itategemea kama Onana ataondoka japo hadi sasa haionekani kama ni rahisi kutokea kwani hakuna ofa kutoka timu yoyote.