Alphonso Davies kukosa mechi ya kwanza Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Marsch amewatoa hofu mashabiki wa Canada kwa kueleza kuwa anatarajia Davies atashiriki michuano hiyo mikubwa duniani huku akikiri kuwa itakuwa vigumu kwa beki huyo machachari kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa kwanza dhidi ya Bosnia na Herzegovina utakaopigwa Juni 12, 2026.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Canada, Jesse Marsch, ametoa taarifa ya kina kuhusu hali ya afya ya nyota wa kikosi hicho, Alphonso Davies ambaye anaendelea kupatiwa matibabu ili kuwahi michuano ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kupata jeraha la misuli mapema mwezi huu.
Marsch amewatoa hofu mashabiki wa Canada kwa kueleza kuwa anatarajia Davies atashiriki michuano hiyo mikubwa duniani huku akikiri kuwa itakuwa vigumu kwa beki huyo machachari kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wa kwanza dhidi ya Bosnia na Herzegovina utakaopigwa Juni 12, 2026.
Kwa sasa, Davies amebaki nchini Ujerumani kuendelea na matibabu maalum chini ya uangalizi wa madaktari wa Bayern Munich, klabu anayoitumikia. Matarajio ni kuanza kuonekana mechi ya pili ya kundi B dhidi ya Qatar (Juni 19) kisha Switzerland (Juni 24).
Marsch amebainisha kuwa, klabu hiyo inatumia teknolojia ya hali ya juu ambayo isingepatikana kwa urahisi endapo angeamua kurejea nyumbani Canada, hivyo ameishukuru Bayern kwa ushirikiano mkubwa wanaouonesha ili kuhakikisha mchezaji huyo anacheza Kombe la Dunia 2026.
Nyota huyo anatarajiwa kuwasili Edmonton, Canada Mei 31, 2026 ili kuungana na kikosi cha timu ya taifa. Baada ya kumaliza matibabu ya awali klabuni ifikapo Mei 28, 2026, Davies atapewa mapumziko ya siku chache kabla ya kuanza rasmi hatua inayofuata ya mazoezi ya kurejesha utimamu wa mwili chini ya benchi la ufundi la Canada.