Alonso: Alivyofaulu mtihani uliowashinda wengi ulaya

Muktasari:

  • Alihitaji misimu miwili tu, kuipeleka Leverkusen katika nchi ya ahadi. Mengi yamesemwa juu ya njia na vitu alivyovibadilisha hadi kuiwezesha timu hii kuwa na ushindani lakini kubwa zaidi ni amefaulu mtihani ambao wengi wameushindwa.

LONDON, ENGLAND: Kwa mara ya kwanza katika historia yao Bayer Leverkusen ilifanikiwa kuchukua taji Bundesliga msimu huu. Kocha aliyesimamia hili ni Xabi Alonso.

Alihitaji misimu miwili tu, kuipeleka Leverkusen katika nchi ya ahadi. Mengi yamesemwa juu ya njia na vitu alivyovibadilisha hadi kuiwezesha timu hii kuwa na ushindani lakini kubwa zaidi ni amefaulu mtihani ambao wengi wameushindwa.

Hapa tumekuletea wachezaji wa zamani watano ambao walipata mafanikio na umaarufu kama ilivyokuwa kwa Alonso lakini walishindwa kufanya vizuri katika ukocha.

5.Wayne Rooney

Rooney amefutwa kazi huko Birmingham City Januari hii baada ya timu kufanya ovyo. Staa huyo aliyekuwa matata kabisa enzi zake akicheza soka, amepoteza ajira yake hiyo na kuiacha Birmingham kwenye nafasi ya 20. Wakati alipokabidhiwa mikoba timu ilikuwa nafasi ya sita Oktoba 2023 na alishinda mechi mbili tu kati ya 15. Aliwahi pia kuifundisha Derby County na D.C. United na kote alichemka.

4.Steven Gerrard

Mwanzoni wakati anaanza ukocha wengi walidhani atakuja kuwa mrithi wa Jurgen Klopp huko Liverpool, lakini baada ya kukabidhiwa kibarua cha kuinoa Aston Villa, Gerrard alichemsha na kushindwa kabisa kufanya kile alichokuwa akifanya akiwa mchezaji. Aston Villa ya sasa imekuwa moto chini ya Unai Emery baada ya yeye kukaribia kuishusha daraja. Yupo Al-Ettifaq ambako hakuanza vizuri ingawa hadi sasa timu hiyo inashika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu Saudi Arabia.

3.Alan Shearer

Kinara wa mabao wa muda wote kwenye Ligi Kuu England ni mkali Shearer. Straika huyo alikuwa matata enzi zake, lakini wakati Newcastle inasaka mtu wa kuwanusuru wasishuke daraja, walimpa kazi Shearer na alichokwenda kufanya ni tofauti kabisa. Shearer alishinda mechi moja tu na kuishusha daraja Newcastle katika msimu wa 2008-09. Makali yote ya wakati anacheza, kwenye ukocha amefeli.

2.Andrea Pirlo

Wakati anacheza, kila kocha alitamani awe na huduma yake kwenye kikosi chake. Pirlo alivutia wengi wakati mpira ulipokuwa kwenye miguu yake na wengi waliamini atakuwa moto atakapohamia kwenye ukocha.

Iliaminika atafanya mambo kuwa mepesi kama ambavyo amekuwa akiamrisha mpira na unamtii. Lakini mambo ni tofauti.

Timu zote alizofundisha alidumu kwa msimu mmoja tu, akianzia Juventus ambako alikaa msimu wa 2020/21, kisha Fatih Karangamuk, msimu wa 2022/23 akafukuzwa na sasa yupo na Sampdoria ambayo inashika nafasi ya nane katika Serie A.

1.Frank Lampard

Akiwa na kikosi cha Chelsea alikuwa mchezaji mwenye sauti na kipenzi cha bosi Roman Abramovic pamoja na mashabiki. Kubwa zaidi hadi sasa ndio anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu hiyo licha ya kwamba alikuwa akicheza nafasi ya kiungo.

Wengi waliamini angeweza kuhamishia makali hayo kwenye ukocha. Baada ya kupewa kazi Derby County na kufika fainali ya play-off, Roman akampa shavu lakuwa kocha wa Chelsea mwaka 2019, mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa na akaishia kuwalaumu sana wachezaji.

Safari yake ikamalizika mwaka 2021, akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi 84, ikashinda 44, sare 15 na kufungwa 25.

Alienda Everton nako mambo hayakuwa mazuri akarudi tena Chelsea kwa mkataba wa muda mfupi msimu wa mwaka juzi nako hali ilikuwa ni vile vile, kwa sasa hana timu.