Alonso agomea dili Olympique de Marseille
Muktasari:
- Alonso, mwenye umri wa miaka 44, alifutwa kazi na Real Madrid, Januari mwaka huu, miezi saba tu tangu alipoondoka Bayer 04 Leverkusen kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Bernabeu.
MADRID, HISPANIA: KOCHA Xabi Alonso amekataa ofa kutoka klabu ya Olympique de Marseille ya Ufaransa, huku tetesi za kurejea kwake Liverpool zikiendelea kushika kasi kuelekea dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Alonso, mwenye umri wa miaka 44, alifutwa kazi na Real Madrid, Januari mwaka huu, miezi saba tu tangu alipoondoka Bayer 04 Leverkusen kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo ya Bernabeu.
Kipigo cha Real Madrid kutoka kwa mahasimu wao wakubwa Barcelona katika fainali ya Spanish Super Cup kiliharakisha kuondoka kwake, ingawa inadaiwa kulikuwa na matatizo ya ndani ya klabu pia.
Inaripotiwa baadhi ya wachezaji wakongwe walihisi kudharauliwa na hawakuridhishwa na falsafa yake ya uchezaji. Uhusiano wake usioridhisha na Vinícius Júnior uliashiria changamoto zake kushinda imani ya vyumba vya kubadilishia nguo.
Rais wa Real Madrid, Florentino Pérez alimfuta kazi haraka na timu imeanza kuimarika chini ya mrithi wake, Alvaro Arbeloa.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Ufaransa, RMC Sport, Alonso alikataa mara moja ofa ya Marseille kutokana na wasiwasi klabu hiyo ya Ligue 1 inaendeshwa katika hali ya vurugu.
Mapema mwezi huu, Roberto De Zerbi alijiuzulu kama kocha baada ya kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Paris Saint-Germain.
Siku nne baadaye, mkurugenzi wa michezo Medhi Benatia alitangaza kuondoka kwenye klabu hiyo akieleza kuwa asingeweza tena kupuuzia hali ya sasa kwenye timu hiyo baada ya kuvunjika kwa mawasiliano kati yake na bodi ya klabu.
Mmiliki wa klabu, Frank McCourt alithibitisha Benatia atasalia katika nafasi yake hadi mwisho wa msimu huu. Katika sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya RC Strasbourg Alsace, mashabiki waliosimama nyuma ya magoli yote mawili walisusia dakika 15 za mwanzo na kuizomea timu yao wakati wa mechi.
Baada ya Alonso kuwakataa, Marseille ilimchagua Habib Beye kuwa kocha wao mpya. Beye, ambaye aliwahi kuichezea Newcastle United na Aston Villa, amechukua mikoba katika Uwanja wa Stade Vélodrome licha ya kufutwa kazi na Rennes wiki iliyopita.
Kuhusu Alonso, kwa sasa anachukua muda kutafakari hatua yake inayofuata, baada ya kuwa mmoja wa makocha waliokuwa wanawaniwa zaidi Ulaya. Amehusishwa na kurejea kwa hisia kali Liverpool kuchukua nafasi ya Arne Slot.