Alexander Isak, Liverpool muda utaamua
Muktasari:
- Tangu alipotua England mwaka 2022 hakucheza mara nyingi huko Merseyside, lakini mara zake chache alizofanya hivyo, amevutiwa na timu hiyo ya Anfield.
NEWCASTLE, ENGLAND: STRAIKA wa Newcastle United, Alexander Isak amekoleza moto wa kuwa kwenye rada za Liverpool huku mwenyewe akiwahi kukiri kuvutiwa na mpango wa kwenda kukipiga huko Anfield.
Tangu alipotua England mwaka 2022 hakucheza mara nyingi huko Merseyside, lakini mara zake chache alizofanya hivyo, amevutiwa na timu hiyo ya Anfield.
Isak alifunga kwenye mechi yake ya kwanza kucheza uwanjani hapo akiwa na kikosi chake cha Newcastle na sasa akili yake ni kujiunga na Liverpool, ambayo imelenga kuvunja rekodi ya uhamisho huko Uingereza ili kunasa huduma yake.
Liverpool tayari imeshatumia Pauni 200 milioni kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini bado haijamaliza, ikitaka kuijaribu Newcastle kwa Isak.
Kinachoelezwa ni Newcastle ipo kwenye wakati mzuri wa kupata ofa yamu kutoka Liverpool, ambayo inaweza kuanzia Pauni 130 milioni kwa ajili ya huduma ya straika huyo matata kabisa Ulaya kwa sasa.
Isak hajawahi kulazimisha kuhama Newcastle, lakini kwa sasa kila kitu kinaonekana kama kitakwenda kutimia baada ya kuondolewa kwenye kambi ya Newcastle.
Liverpool wanafahamu vyema ubora wa mshambuliaji huyo, ambaye aliwafunga msimu uliopita, wakati Newcastle United iliponyakua taji la Kombe la Ligi.
Kikosi hicho cha kocha Arne Slot kimeshavunja rekodi kwenye dirisha hili wakati ilipomnasa kiungo wa Kijerumani, Florian Wirtz kwa ada ya Pauni 116 milioni, lakini usajili wa Isak, unaweza kuvunja rekodi hiyo na kuandika mpya kwenye soka la England. Ofa ya Liverpool inaweza kufikia Pauni 130 milioni, lakini Newcastle inamthaminisha straika wao huyo kuwa na thamani ya Pauni 150 milioni.