Alexander Isak ajadiliwa atabaki, habaki

Muktasari:
- Hata hivyo, kiungo wa zamani wa Sunderland, Bolo Zenden anadai anaamini Isak hatakuwa na mpango wa kuachana na Newcastle hata kama timu hiyo itashindwa kufuzu michuano ya Ulaya.
LONDON, ENGLAND: HATIMA ya straika Alexander Isak kwenye kikosi cha Newcastle United itategemea majaliwa ya timu hiyo kama itafuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Isak, 25, amekuwa straika anayesakwa sana sokoni kwa sasa, huku Arsenal na Liverpool zote zikionyesha wazi kuhitaji huduma yake na huenda zikachuana vikali kumnasa dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Isak amekuwa na msimu bora kabisa, akifunga mabao 21 na kuasisti mara tano kwenye mechi 30 alizocheza kwenye michuano yote, ikiwamo mabao aliyofunga dhidi ya Arsenal Ligi Kuu England na Kombe la Ligi.
Newcastle haipo tayari kuachana na straika wao huyo dirisha lijalo majira ya kiangazi na ndiyo maana imetaja bei yake inaanzia Pauni 150 milioni na ipo kwenye mchakato wa kumsainisha dili jipya litakalomfanya adumu kwenye kikosi hicho kwa zaidi ya mwaka 2028.
Wakati ikifanikiwa kubaki naye dirisha la Januari, straika wa zamani wa Ligi Kuu England, Emile Heskey anaamini Newcastle itafanikiwa kubaki na mchezaji huyo kama tu itafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Fowadi huyo wa zamani wa Liverpool na England, Heskey, anaamini lazima kutakuwa na makubaliano maalumu baina ya Isak na mabosi wa Newcastle atafungasha virago vyake na kuondoka endapo timu hiyo itashindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, kiungo wa zamani wa Sunderland, Bolo Zenden anadai anaamini Isak hatakuwa na mpango wa kuachana na Newcastle hata kama timu hiyo itashindwa kufuzu michuano ya Ulaya.
Anaamini kucheza michuano yoyote ya Ulaya kama Europa League hiyo ni tosha kwa Isak kuzikataa Arsenal na Liverpool ili kubaki kwenye mazingira ambayo amezoea kufanya kazi.