Aguero huyoo PSG kwa Pochettino

Saturday January 09 2021
ANASEEPA PIC

Paris, Ufaransa. Kocha wa PSG, Mauricio Pochettino anamuwinda nyota wa Manchester City, Sergio Aguero ili amnase katika dirisha kubwa la usajili mwishoni mwa msimu.

Wakala wa mchezaji huyo, Bruno Satin amefichua kuwa Pochettino anavutiwa vilivyo na Aguero ambaye ni mmoja ya washambuliaji wenye uwezo wa hali ya juu wa kufumania nyavu.

ANASEPA PIC2

Mkataba wa Aguero na Manchester City umebakiza miezi sita na pande hizo mbili bado hazijafikia makubaliano ya kuurefusha.

Na sasa Satin ambaye anawasimamia pia, Olivier Giroud na Michael Landreau amefichua kuwa Pochettino amemuweka Aguero katika orodha ya vipaumbele vyake kwenye usajili ujao wa majira ya kiangazi.

Huku hatima yake ikiwa haieleweki ndani yaCity, Aguero kwa sasa anaruhusiwa kufanya mazungumzo na hata kusaini mkataba wa awali na timu nyingine.

Advertisement

Satin amedai kuwa PSG wako tayari kumlipa nyota huyo wa Argentina kiasi cha Pauni 240,000 kwa wiki ambacho amekuwa akilipwa na Manchester City ili aweze kuhamia Ufaransa aungane na Pochettino aliyejiunga na timu hiyo wiki iliyopita kuchukua mikoba ya Thomas Tuchel aliyetimuliwa.

ANASEPA 3

Majeruhi ya mara kwa mara yameonekana kumuathiri Aguero ambaye amejikuta akicheza mechi tano tu msimu huu jambo ambalo linawapa hofu Manchester City kumpa mkataba mpya wakihofia wanaweza kupata hasara.

Lakini pamoja na hilo, kocha wa City, Pep Guardiola amekuwa akisisitiza kuwa klabu hiyo itahakikisha inaendelea kubakia na Aguero ingawa ina wasiwasi juu ya uwezo wake.

“Tunajua anamaanisha nini kwetu. Tunajua ni kwa jinsi gani tunamthamini ila anatakiwa kutuonyesha kila mmoja wetu wa kwanza nikiwa mimi kwamba tunatakiwa kuendelea kuwepo hapa, kucheza vizuri na kushinda mechi.

Baada ya hapo, klabu pamoja na mimi tunatakiwa kuamua kuhusu ubora wake. Pindi akicheza katika kiwango chake hatuna shaka kwamba ni mchezaji anayetakiwa kubaki hadi pale atakapoamua kuondoka. Ni mchezaji wa kipekee. Ni muhimu kwetu, kwa mashabiki na kwa kila mmoja,” alisema Guardiola.

Mchambuzi wa soka, Micah Richards ambaye amewahi kucheza pamoja na Aguero amesema anategemea kuona mshambuliaji huyo akiongeza mkataba mpya wa kuitumikia Manchester City.

“Lengo lake siku zote limekuwa ni kumalizia soka Argentina ila nategemea kwa sasa Pep Guardiola amesaini mkataba na Aguero atafanya kama hivyo.

Iwe kwa miezi 12 au miaka miwili, ni aina ya biashara ambayo naamini City wataikamilisha,” alisema Richards.

Advertisement