Achraf Hakimi wa nini, kuna Mazraoui
Muktasari:
- Katika mechi hiyo ya Jumapili, Morocco iliziba pengo la Hakimi kwa kumpanga beki wa Manchester United, Mazraoui kwenye nafasi hiyo ya beki wa kulia na mambo yalikwenda vizuri kabisa.
CASABLANCA, MOROCCO: BEKI wa kulia, Achraf Hakimi ameshindwa kucheza mechi ya kwanza ya Afcon 2025, lakini hilo la kukosekana kwake wala halikuwa pengo kwenye kikosi cha Morocco baada ya uwepo wa Noussair Mazraoui, aliyepiga mzigo si kitoto.
Kocha wa Morocco, Walid Regragui, ambaye alishuhudia timu yake ikiiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Comoro katika mechi hiyo ya ufunguzi iliyofanyika Jumapili, amesema kukosekana kwa beki wa kulia, Hakimi, ambaye ni Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika, haikuwa shida kabisa kikosini.
Katika mechi hiyo ya Jumapili, Morocco iliziba pengo la Hakimi kwa kumpanga beki wa Manchester United, Mazraoui kwenye nafasi hiyo ya beki wa kulia na mambo yalikwenda vizuri kabisa.
Mabao ya Brahim Díaz na Ayoub El Kaabi yalihakikishia Morocco ushindi wa mabao 2-0 katika kipute hicho kilichofanyika uwanjani Prince Moulay Abdellah. huku wenyeji hao walikosa penalti kwenye kipindi cha kwanza.
Katika mechi hiyo, Mazraoui aliasisti bao la kwanza la Morocco, lililofungwa na Diaz kwenye dakika 55.
"Bila ya Hakimi tulikuwa na wasiwasi wa kufanya vizuri, lakini Mazraoui alikuwa bora," amesema Regragui.
"Namweka kwenye anga zile zile za wachezaji makini kama Achraf, licha ya kwamba kiwango chake ni tofauti.
"Bado tunamhitaji Hakimi, yeye ni mmoja wa wachezaji bora wa Afrika na duniani, hakuna timu duniani ambayo haitaki kumchezesha mchezaji wao bora. Staili ya mechi hii ilimfaa zaidi Hakimi, angetusaidia kutokea pembeni."
Hakimi, 27, hajacheza tangu alipoumia enka ya kushoto wakati akiitumikia Paris Saint-Germain kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich na sasa anapambana kwa nguvu zote kupona majeraha yake ili kurudi kwa haraka kucheza mashindano ya Afcon 2025 yanayofanyika kwenye ardhi ya kwao huko Morocco.
"Tutaangalia hali itakavyokuwa ndani ya saa 48, tuone kama tunaweza kumwaanzisha dhidi ya Mali," amesema Regragui.
Kurejea kwa Hakimi kutamfanya kocha Regragui kuwa kwenye wakati mgumu kutokana na Mazraoui na beki wa kushoto Anass Salah-Eddine, ambaye aliasisti bao la El Kaabi, aliyefunga kwa ticktack wote kufanya vizuri dhidi ya Comoro.
"Nina mabeki wa pembeni matata; Salah-Eddine yupo kwenye viwango bora kabisa upande wa beki ya kushoto na Mazraoui naye yupo kwenye nafasi bora ya kiufundi," amesema Regragui.
Morocco iliyopangwa kwenye Kundi A itashuka uwanjani tena kukabiliana na Mali mjini Rabat, Desemba 26, kabla ya kukamilisha hatua ya makundi kwa kukipiga na Zambia siku tatu baadaye.