Acha tuone Foden na Bruno nani mwamba fainali FA

Muktasari:

  • Kama kawaida, kwenye kipute hicho cha Wembley, mshindi ni mmoja tu. Ni nani?

LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Manchester City na Manchester United kinapigwa kesho Jumamosi kwenye fainali ya Kombe la FA, ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo.

Kama kawaida, kwenye kipute hicho cha Wembley, mshindi ni mmoja tu. Ni nani?

Man City ndiyo iliyoibuka na ushindi kwenye fainali hiyo mwaka jana. Safari hii, itakuwaje?

Ilkay Gundogan alifunga bao la haraka zaidi kwenye historia ya Kombe la FA wakati alipotumia sekunde 12 tu kutikisa nyavu kwenye fainali ya mwaka jana.

Bruno Fernandes aliisawazishia Man United kabla ya mapumziko kwa mkwaju wa penalti. Lakini, Gundogan ndiye aliyekuwa na mtu wa kauli ya mwisho kwenye mechi hiyo, wakati alipofunga bao la pili kuipa Man City ushindi wa 2-1 na hivyo kunyakua kombe hilo, msimu ilionyakua mataji matatu.

Safari hii, hakutakuwa na mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Man City, hivyo nguvu zote zimeelekezwa kwenye fainali hiyo ya Kome la FA huko Wembley.

Kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola tayari kimeshabeba taji la Ligi Kuu England, ikiwa ni msimu wa nne mfululizo. Miamba hiyo ya Etihad bila ya shaka inachotaka ni kunyakua taji hilo la pili msimu huu.

Kwa upande wa Man United, yenyewe inalihitaji zaidi taji hilo la Kombe la FA.

Kikosi hicho cha Kocha Erik ten Hag kimemaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, nafasi ya chini zaidi kuwahi kuikamatia kwenye ligi hiyo, hivyo hawatakuwapo kwenye michuano yoyote ya Ulaya.

Kama Man United itashinda leo Jumamosi, itakuwa imeweka kwenye mkoba tiketi ya kucheza Europa League, hivyo itaifanya Chelsea kupoteza tiketi kwenye michuano hiyo na kuhamia Conference League na hapo, Newcastle United itakuwa imemaliza mikono mitupu na hakutakuwa na soka la Ulaya msimu ujao.

Ushindi pia unaweza kuokoa kibarua cha Ten Hag, huku kipigo kinaibua mashaka huenda ikawa mwisho wa kocha huyo Mdachi kwenye ajira yake huko Old Trafford baada ya kufanya kazi hapo kwa miaka miwili.

Man United haipaswi kujiamini sana baada ya kukaribia kutupwa nje kwenye hatua ya nusu fainali, iliposhinda kwa mikwaju ya penalti dhidi ya timu ya Championship, Coventry City.


Viwango vyao vipoje?

Ukiweka kando kuondolewa kwao kwa mikwaju ya penalti na Real Madrid kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Man City haijapoteza mechi ndani ya dakika 90 katika mechi 35 za mwisho.

Ipo kwenye ubora mkubwa, ikiwa imeshinda mechi sita mfululizo na hali ya kujiamini ipo juu sana.

Kwa upande wa Man United imemaliza msimu kwa kushinda dhidi ya Newcastle na Brighton.

Lakini, kabla ya mechi hizo, Man United ilikumbana na kichapo kutoka kwa Crystal Palace na Arsenal na safu yao ya ulinzi imeonekana kuvuja kuzidi maelezo.


Mambo ya timu

Man City inajipanga kuwa na karibu kikosi chao kizima kikiwa fiti kwa ajili ya fainali hiyo.

Mchezaji pekee ambaye hatakuwapo kwenye kikosi hicho cha Guardiola ni kipa Ederson, ambaye aliumia mfupa wa jicho kwenye mechi dhidi ya Tottenham. Hiyo ina maana, Stefan Ortega ataendelea kukaa golini.

Mastaa Jack Grealish na Nathan Ake wanatarajia kuwa fiti kwa ajili ya mchezo huo. Ni hao ndiyo wachezaji wanaotia mashaka kwenye kikosi cha Man City, lakini wengine wote wapo fiti kwa mechi.

Wakati huo, Man United yenyewe ina matumaini ya kumkaribisha kikosi beki wa kati Harry Maguire baada ya kukosa mechi za mwisho wa msimu kutokana na kuwa majeruhi.

Kuna hatihati pia kuhusu beki Luke Shaw, huku Anthony Martial, Victor Lindelof na Mason Mount nao wanaweza kufuzu mtihani wa kuwa fiti na kupewa dakika chache za kucheza kwenye kipute hicho cha Wembley. Lakini, Tyrell Malacia atakosa mechi, kutokana na beki huyo wa kushoto kutarajia kurudi uwanjani Julai.


Mastaa wa kuchungwa

Man City inaweza kukuadhibu kupitia yeyote na muda wowote. Lakini, ni ngumu sana kumwona Phil Foden asifanye yake ndani ya uwanja kutokana na kiwango chake matata kabisa msimu huu, akishanguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka kwenye Ligi Kuu England.

Kwa Man United, yenyewe pia ina mastaa tishio wanaoweza kuleta kasheshe muda wowote. Lakini, kiungo Bruno Fernandes anaendelea kuwa mchezaji muhimu wa kikosi hicho cha Old Trafford, hivyo inamhitaji awe kwenye kiwango bora kuwa na nguvu ya kuwakabili Man City.


Makocha wamesemaje?

Pep Guardiola: “Nilianza kufikiria hakukuwa na mtu aliyewahi kushinda mara nne mfululizo. Hilo limekwisha na kinachofuata ni Kombe la FA. Gary Lineker aliniambia hakuna timu iliyowahi kushinda Ligi Kuu England na Kombe la FA kwa misimu miwili mfululizo.

“Ninachotaka kwa wachezaji wangu wapate mapumziko ya siku mbili au tatu kujiandaa na fainali.”

Erik ten Hag: “Safi. Fainali ya Kombe la FA. Ni tukio kubwa. Ukiwa mtoto, unataka kuwa sehemu ya vitu hivi. Kila mtu anavutiwa na kushinda kombe hili.

“Bado tuna nafasi nzuri, kwenda kupata mafanikio kwenye fainali na ni mechi unayohitaji kushinda. Ni suala la makombe na tuna nafasi ya kulinyanyua. Tunahitaji pia kucheza Ulaya, hii ni nafasi yetu ya mwisho.”


Umebeti?

Man United mara zote zimekuwa ikijiandaa kwa mechi hiyo ya mahasimu, hasa kwa umuhimu wa mchezo huo wa Man City kw aupande wao katika msimu huu.

Lakini, kubeba mataji mawili ndani ya msimu mmoja, ndicho kitu kinachoonekana kuwa na nafasi kubwa ya kutokea kwenye fainali hiyo kwa maana ya Man City kuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Straika Erling Haaland bila ya shaka atafanya jambo mbele ya beki ya hovyo ya Man United.

Kitu kingine ni Man United kupata shida kufunga mabao, hivyo kinachoonekana Guardiola atakwenda kumtambia mpinzani wake, Ten Hag katika mchezo huo wa fainali.