Man United, kuvunja mkataba wa Amorim itawakosti Sh 65B
Muktasari:
- Kocha huyo wa Man United inaelezwa kwamba kwenye mkataba wake kumewekwa kipengele kinachofichua — atalazimika kulipwa malipo yake ya miaka miwili na nusu itakayokuwa imebaki endapo atafutwa kazi.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United italazimika kulipa fidia ya Pauni 12 milioni endapo kama itaamua kumfuta kazi kocha Ruben Amorim mwishoni mwa msimu huu.
Kocha huyo wa Man United inaelezwa kwamba kwenye mkataba wake kumewekwa kipengele kinachofichua — atalazimika kulipwa malipo yake ya miaka miwili na nusu itakayokuwa imebaki endapo atafutwa kazi.
Hakuna namna yoyote inayomfanya bilionea Sir Jim Ratcliffe amfute kazi Mreno huyo bila ya kulipa fidia. Amorim alijiunga na Man United, Novemba mwaka jana kuchukua mikoba ya Erik ten Hag.
Amorim hana rekodi ya kuvutia tangu alipotua Man United, ambapo katika mechi 15 alizoiongoza timu hiyo kabla ya mchezo wa usiku wa Jumatano dhidi ya Ipswitch Town uwanjani Old Trafford, alishinda nne tu na kupotena nane. Kocha huyo alikiri kuinoa Man United mbovu zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya timu hiyo.
Kiwango hicho cha pesa kiliwekwa kwa benchi lote la Amorim alipojiunga na timu hiyo ili kuweka usalama kwa watu wake aliotua nao kutoka Sporting.
Kwa maana hiyo, Man United itakapoamua kumfuta kazi Amorim na benchi lake lote, italazimika kulipa Pauni 20 milioni, sawa na Sh65.6 bilioni za Kitanzania. Wiki iliyopita, hesabu za Man United hadi kufikia mwisho wa 2024 zilionyesha timu hiyo kuwa na deni la Pauni 1 bilioni, ikiwamo Pauni 300 milioni za ada za usajili ambazo imekuwa ikilipa kidogo kidogo. Ripoti nyingine inafichua kwamba klabu zenye wachezaji kutoka Man United ambao waliwekewa vipengele vya timu hiyo ya Old Trafford kupata mgawo wa kifedha endapo watauzwa, wanataka kuvinunua vipengele hivyo. Baadhi ya wachezaji hao ni Scott McTominay, Mason Greenwood, Facundo Pellistri na Hannibal Mejbri. Kwenye hatua nyingine, bilionea Sir Jim Ratcliffe amepanga kupunguza wafanyakazi 200, ukiweka kando wale 250 waliofutwa mwaka jana ili kuimarisha vitabu vya kifedha vya timu hiyo isiingie kwenye matatizo na mamlaka.