Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KIPIGO CHA GHARAMA: Man City yatupwa nje CWC, Guardiola atoa neno

Muktasari:

  • Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kilianza vyema kwenye mechi hiyo iliyopigwa Orlando, Florida. Bao la mapema la Bernardo Silva liliwapa uongozi kabla ya kukosa nafasi kadhaa za wazi kabisa za kufunga huku ikicheza kwa kiwango bora kwenye kipindi cha kwanza.

FLORIDA, MAREKANI: MANCHESTER City imetupwa nje ya fainali za Kombe la Dunia la Klabu baada ya kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa miamba ya Saudi Pro League, Al-Hilal katika mchezo wa mtoano hatua ya 16 bora.

Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kilianza vyema kwenye mechi hiyo iliyopigwa Orlando, Florida. Bao la mapema la Bernardo Silva liliwapa uongozi kabla ya kukosa nafasi kadhaa za wazi kabisa za kufunga huku ikicheza kwa kiwango bora kwenye kipindi cha kwanza.

Al-Hilal ilipambana kipindi cha pili na kufunga mara mbili kupitia kwa Marcos Leonardo na Malcom, kabla ya Man City kusawazisha kwa bao la Erling Haaland na kufanya mechi hiyo kuingia kwenye dakika 30 za nyongeza ili kuwa 120, ndipo Al Hilal ilipofunga mara mbili zaidi, kupitia kwa Kalidou

Koulibaly na Leonardo, akifunga bao lake la pili kwenye mchezo dakika 112, huku Man City ilifunga mara moja kwenye dakika hizo kupitia kwa Phil Foden.

Lakini, Man City kutupwa nje imewagharimu pesa kiasi gani? Kwa kucheza mechi nne kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu tayari ilikuwa biashara nzuri kutokana na pesa ambazo Man City itavuna, lakini kutolewa mapema kumewagharimu pakubwa kiuchumi.

Kwa kushindwa kwanza kutinga hatua ya robo fainali, hilo limewafanya Man City kupoteza Pauni 9 milioni. Kabla ya mechi hiyo kuanza, Man City ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kusonga hatua inayofuata mbele ya wapinzani wao hao wa Saudi Arabia.

Miamba mingine ya Ulaya iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kusonga mbele ni PSG, Bayern Munich na Real Madrid huku Inter Milan ikitupwa nje baada ya kichapo kutoka kwa Fluminense.

Lakini, Man City ilikumbana na jambo la kuduwaza kutoka kwa timu isiyokuwa ya Ulaya – Al-Hilal na kama ingevuka hapo, basi ingekutana na Fluminense kwenye hatua ya robo fainali na ama Chelsea au Palmeiras kwenye hatua ya nusu fainali.

Kwa kitendo cha kushindwa kufika nusu fainali, Man City imepoteza fursa ya kuvuna Pauni 16.2 milioni. Na ingevuna mkwanja zaidi, Pauni 23.2 milioni endapo kama ingefanikiwa kufika fainali, ambayo itapigwa huko New Jersey, Julai 13. Kushinda ubingwa, kungewapa Pauni 30 milioni.

Kama pesa zote hizo zikijumlisha, Man City ingeondoka kwenye fainali hizo na mkwanja wa Pauni 78 milioni, lakini kwa kutupwa nje mapema imepoteza fursa hiyo.

Kuonyesha mambo yalivyokuwa tofauti, Man City iliwekeza Pauni 109 milioni kwa kusajili wachezaji watatu kwa ajili ya fainali hizo, Rayan Ait-Nouri, Rayan Cherki na Tijjani Reijnders.

Kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia la Klabu kungepunguza machungu ya matumizi ya pesa hizo hasa ukizingatia Pauni 37.8 milioni ambazo Man City imeshavuna kwa kushiriki michuano hiyo kwenye hatua ya makundi na 16 bora.

Kocha Guardiola alisema: Inasikitisha sana. Tulikuwa vizuri na hamasa ilikuwa kubwa kwenye kikosi. Sijui niwashukuru vipi wachezaji kwa namna walivyofanya mazoezini na jinsi walivyocheza. Lakini, hii ilikuwa mechi ngumu. Tofauti ilikuwa ndogo sana. Tulitengeneza nafasi nyingi na kipa wao Yassine Bounou aliokosa sana. Tungependa sana kuendelea, kwa sababu hii inakuja mara moja kila baada ya miaka minne, lakini sasa tunakwenda nyumbani kupumzika – akili yetu inaelekea msimu ujao.