Emery afunga mjadala kuhusu Mesut Ozil

LONDON ENGLAND. KOCHA wa Arsenal, Unai Emery amesema amepata baraka zote kutoka kwa mabosi wa timu hiyo juu ya kumpiga chini kiungo Mesut Ozil.

Kiungo huyo anayelipwa mshahara mkubwa kuliko mchezaji yeyote kwenye kikosi cha Arsenal amekuwa kwenye wakati mgumu tangu Kocha Emery alipojiunga na timu hiyo ambapo kwa msimu huu alianzishwa mara mbili tu huku mara ya mwisho kuonekana kwenye kikosi ilikuwa Septemba.

Mashabiki wa Arsenal walisikika wakiimba wimbo wa kutaja jina la Ozil baada ya kikosi hicho kuonyesha kiwango kibovu kwenye mechi zao mbili zilizopita. Jana Jumapili, Arsenal ilitarajia kukipiga na Crystal Palace kwenye Ligi Kuu England.

Ozil aliwekwa nje ya kikosi katika mechi zote mbili zilizopita, ile waliyopigwa na Sheffield United kwenye Ligi Kuu England Jumatatu iliyopita na ile waliyoshinda kwa mbinde dhidi ya Vitoria kwenye Europa League, Alhamisi iliyopita.

Kocha Emery haonekani kuwa tayari kuwasikiliza mashabiki na kuanza kumtumia staa huyo, ambaye huko nyuma aliwahi kusema kwamba hastahili kupata nafasi ya kucheza mbele ya makinda wanaonekana kuwa moto zaidi.

Emery alisema: “Huko nyuma, tulifanya mazungumzo na kufikia uamuzi. Kulikuwa na makubaliano baina ya klabu kama timu, kwa sababu kitu muhimu ni klabu na kisha kinafuata kiwango cha mchezaji.”

Moja ya mechi ambazo mashabiki wa Arsenal walisikika wakiimba jina la Ozil ni ile dhidi ya Vitoria iliyopigwa uwanjani Emirates, ambapo Arsenal ilisubiri hadi mabao mawili ya friikiki ya mtokea benchi, Nicolas Pepe kuwaokoa na kupata ushindi wa mabao 2-3 baada ya kutanguliwa nyumbani.