Zarika amtaka Fatuma ulingoni

TETESI za awali zilizozagaa kama moto mkali kwenye kichaka kikavu eti bondia wa kike nchini Fatuma ‘Iron Fist’ ameangika glavu zake ukutani ni hot air tu mazee!
Akiongea na Mwanaspoti, Zarika alisema bado yupo katika gemu na anapania kurudi kinyama ulingoni kutetea mkanda wake wa World Boxing Federation (WBF) uzani wa Super Feather.
Zarika ameratibiwa kutwangana na Fatuma Omari kutoka Bongo ambaye tofauti na mwenzake Karim ‘Mtu Kazi’ Mandoga, amekuwa baridi kuzungumzia pigano hilo.
Lakini Zarika alisema wala hana muda wa kucheka na mpinzani wake katika pigano hilo la raundi 10 litakaloandaliwa katika ukumbi wa Broadwalk Mall, Parkland jijini Nairobi.
“Nitamvuruga kuanzia mwanzo kuhakikisha mkanda unasalia nchini, nawaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia nitakavyomcharaza Mbongo huyo,” alijichocha Zarika.
Promota wa pigano hilo Maurice Odera wa Utra Fight Series Boxing alisema kila kitu kipo shwari huku akiwahimiza mashabiki kujitokeza kushuhudia burudani hili.
Zarika alishinda mkanda huo Novemba mwaka 2020 baada ya kumcharaza Patience Mastara wa Zimbabwe kwa wingi wa pointi katika pigano lililoandaliwa nchini Tanzania.
Bingwa huyu wa zamani mkanda wa World Boxing Commission (WBC) uzani wa bantam anayejifua chini ya kocha Marvin Abuya amesema pigano hilo litamfungulia milango ya kuwania tena taji lake la WBC.
Zarika amepigana mara 48 akishinda mapigano 33 ambapo kati ya hizo, 17 ni kwa njia ya knockout huku akiwa amepoteza mapigano 13 na kuandikisha matokeo ya sare mara mbili.
Naye Fatuma amepanda ulingoni mara 31 akishinda mapigano 20 huku 10 zikiwa kwa KO, na sare ikiwa moja.