Wanyama anaihata Harambee Stars

NAHODHA wa zamani wa Harambee Stars, Victor Mugubi Wanyama anatamani tena kurejea kwenye kikosi  hicho licha ya kutangaza kustaafu kimataifa.
Kulingana naye mwenyekiti wa zamani wa FKF tawi la Mombasa, Twaha Mbarak aliyetangaza nia yake ya kugombea Urais wa FKF, Wanyama kamfungulia roho na kumfahamisha kuwa angelipenda kurudi kwenye kikosi hicho.
Mbarak ambaye amekuwa akiendelea na mchakato wa kusaka sapoti ya wadau mbalimbali, alikutana na Wanyama huko jijini Montreal, Canada anakoishia kiungo huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs akiichezea Montreal FC.
Licha ya  kutangaza kustaafu soka la kimataifa Oktoba 2021 baada ya kutemwa na makocha Jacob Ghost Mulee na Francis Kimanzi, Wanyama kakiri kwake Mbarak kuwa anaihata sana timu hiyo aliyoitumikia kwa miaka 14 akiichezea jumla ya mechi 52 na kupachika magoli saba.
"Nilikutana na Wanyama hivi majuzi nyumbani kwake Montreal, Canada na tukazungumza sana. Hofu yake kubwa ni mwelekeo wa soka la Kenya kwa sasa. Aliniambia angependelea sana kuona utata wa kiuongozi uliopo ukitatuliwa haraka sana na Kenya kuondolewa kwenye marufuku. Kwa maana hiyo anahisi ni jukumu la Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohammed kujitahidi kufanya majadiliano na FIFA ili kumaliza utata uliopo," Mbarak kasema.
Kando na mustakabala wa soka nchini ambalo kwa sasa linaongozwa na kamati ya mpito, Mbarak anasema pia alimhoji Wanyama kuhusu malengo yake ya usoni kabla hajastaafu soka rasmi.
"Nilimuliza kama angependa kurudi kwenye timu ya taifa sababu bado ninamwona ana nguvu na ingawaje alisitasita, niliona kabisa anaihata Stars na angependelea kurejea. Ana mapenzi makubwa na kikosi hicho na kwamba anamisi kuichezea. Ila aliniambia kwa sasa hawezi kunijibu rasmi kutokana na kinachoendelea kwenye soka letu, ila ni wazo ambalo atalifanyia kazi"
Alipotangaza kustaafu, Wanyama alikiri wazi kwamba haukuwa uamuzi rahisi wake kuifanya.
Wanyama alitangaza kustaafu baada ya kupokonywa unahodha na kisha kuachwa nje kwa takriban mechi tano za kimataifa hata pale alipokuwa fiti.