Walia Bandari kukosa Mapinduzi Cup

WADAU wa soka wamesikitishwa na kitendo cha Bandari FC kunyimwa ruhusa kushiriki michuano ya kila mwaka ya Mapinduzi Cup inayoendelea visiwani Zanzibar ambapo wangepata fursa kutunishana misuli na miamba ya soka Bongo, Yanga na Simba.

Mkurugenzi wa Ufundi Cosmos FC, Aref Baghazally, aliinyooshea kidole cha lawama Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuwafungia mlango Bandari FC kusafiri kwenda Zanzibar.

“Ni masikitiko makubwa kwa wachezaji wa timu yetu ya Bandari kukosa fursa ya kuonyesha ubora wao na kupata uzoefu wa kucheza na klabu maarufu ukanda huu wa Afrika Mashariki,” alisema Baghazally.

Alisisitiza FKF haijaitendea haki Bandari FC kwasababu mashindano hayo ni wiki mbili na yasingevuruga ratiba ya FKFPL kwa gemu zinazohusu Bandari FC.

Naye mdau mwingine wa soka Pwani ambaye pia ni shabiki shakiki wa Bandari FC, Awadha Karama kutoka Kongowea, alidai Bandari FC kunyimwa kwenda Zanzibar ni mbinu za kuihujumu timu hiyo pekee ya Pwani inayokipiga FKFPL.

Naye Amir Salim alihoji kivipi ushiriki wa Bandari FC mashindano ya Mapinduzi Cup yangeivuruga ratiba ya FKFPL kwasababu wangekosa mechi mbili tu kwani mashindano hayo yanachezwa kipindi ligi imechukua mapumziko.