Wachezaji wa kike wa Kenya kukimbilia Tanzania, ni pesa au kujitangaza?

NAIROBI. KWA miaka ya karibuni, soka la Tanzania limekua kwa kasi. Hii imetokana na uwekezaji mkubwa unaliofanywa na unaoendelea kufanywa na wadau wengi wa mchezo huo.

Kuanzia miundombinu hadi wachezaji, uwekezaji umefanywa na maendeleo yanaonekana.

Kwenye soka la wanawake hawajaachwa nyuma. Timu zinazoshiriki ligi mbalimbali na hasa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) imekuwa na mvuto na wachezaji wengi kutopka mataifa mbalimbali wanaikimbilia.



Kwa nini? Fursa ya kupata pesa ni kubwa.

Wakenya hawajaachwa mbali. Wengi wamekimbilia Tanzania kusaka maisha. Ligi Kuu ya Wanawake ndio kimbilio lao.

Mishahara na pesa za usajili inatajwa ndio sababu kubwa ya Wakenya wengi kukimbilia Bongo.

Dili nono za mikataba imekuwa moja ya vishawishi vikubwa kuwafanya wanasoka wa kike wa Kenya kukimbilia Tanzania. Sio hao tu, mataifa kama, Uganda, Nigeria, Marekani, kuna wachezaji wake huko.

Ligi ya Bongo imekuwa kivutio kwa wachezaji wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF-WPL) na wa Harambee Starlets kwenda kujitafutia unga.

Sababu kubwa inayotajwa ni ukosefu wa malipo na rasilimali kumesukuma wachezaji wengi wenye talanta kuvuka mpaka. Ingawa hii inaonyosha ubora wa wachezaji wa FKF-WPL, inazua wasiwasi kuhusu hali ya soka la wanawake nyumbani.

Mwaka 2020, wakati wa janga la Covid-19, wanasoka 31 wa kike wa Kenya waliondoka kwenye klabu zao vya FKF-WPL na kutorokea vilabu nje ya nchi.

Washambuliaji Jentrix Shikangwa, Topister Situma, Cynthia Shilwatso, kiungo Corazone Aquino, mabeki Esther Amakobe na Ruth Ingotsi waliondoka kwenda kujitangaza kisoka.

Wakati huo, Shilwatso na Amakobe walijiunga na Fountain Gates Princess, huku Situma, Shikangwa, Ingotsi, na Aquino wakijiunga na Wekundu wa Msimbazi, Simba Queens.

Beki Dorcus Shikobe Nixon na kiungo Ivy Faith walijiunga na timu ya Ligi Kuu ya Wanawake ya India SETHU FC, na Violet Nanjala alijiunga na Municipal de Laayoune Women, Morocco.

Katika uhamisho wa hivi majuzi wa Desemba mwaka jana, kiungo wa Starlets, Elizabeth Wambui alihamia Simba akitokea Gaspo Women ya FKF-WPL.

Kiungo mwingine Janet Moraa Bundi kutoka Vihiga Queens na mshambuliaji Airine Madalina wa Bunyore Starlets walijiunga na Yanga Princess Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu mtawalia.


Madalina, 21, alikuwa mfungaji bora wa FKF-WPL msimu wa 2022/23, akiifungia Bunyore mabao 18. Katika mechi yake ya kwanza akiwa na Yanga Januari 10, 2024, alifunga bao la pekee la ushindi dhidi ya Fountain Gate Princess.

Kabla ya kuondoka Vihiga, Bundi pia alikuwa mfungaji bora wa ligi, akiwa amefunga mabao manne katika mechi tano. Kwa sasa amefungia Watoto wa Jangwana mabao mawili katika mechi nne

"Nipo kwa sababu za kifedha na kupata fursa ya kuonyesha talanta yangu. Ligi ya Tanzania inajulikana kwa aina yake ya uchezaji, ambayo ni tofauti na ligi ya nyumbani. Lengo langu ni kuandikisha historia hapa,” alisema Bundi aliyesaini mkataba wa miaka miwili na Yanga.

Mshambuliaji Shikangwa pia alirejea Simba Queens mwezi huu kwa mkataba wa miezi sita, akitokea Beijing Professional FC ya China baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa miezi sita.

Hata hivyo, alichagua kurejea nyumbani Kenya kwani alitarajia kupata klabu nyingine nje lakini, yote hayakwenda sawa. Timu ya FKF-WPL ya Kenya Police Bullets FC ilitaka huduma yake lakini alikataa ofa hiyo na kuchagua kurejea Simba.

"Simba sasa ni nyumbani. Nilikaribishwa kwa moyo mkunjufu. Uwepo wa Wakenya wenzangu umerahisisha mambo na pamoja na wachezaji wenzangu, tutaisaidia timu kusajili matokeo mazuri. Klabu iliweka ofa nzuri mezani na kwa kuzingatia asili ya taaluma yangu na hitaji la uthabiti wa kifedha, nilikubali," Shikangwa aliliambia Mwanaspoti baada ya kusaini mkataba huo Januari 11, 2024.

Mchezaji huyo wa zamani wa Vihiga na timu ya Fatih Karagumruk ya Uturuki,  alijizolea umaarufu mkubwa nchini Tanzania msimu uliopita, akiifungia Simba mabao 17 katika mechi 16 na kumfanya kuwa mfungaji bora.

Licha ya Simba kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, pia alitambuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Msimu.

"Tulitoka nyumbani kwenda kutafuta riziki, soka Kenya hailipi kabisa. Sisi tuko kazini na pia tunajijengea jina. Hapa wachezaji wanalipwa marupurupu ya mechi na mishahara kwa wakati,” alibainisha Wambui.

Katika ligi ya Kenya, wachezaji wanalipwa tu kupitia posho za mechi, ambazo zinaweza kufikia Tsh8,000 hadi Tsh30,000 siku za mechi, huku baadhi ya wachezaji wakipokea hiyo kama mishahara yao ya kil a wiki.                  

Hali hii inadhihirishwa na Yanga, wachezaji wanaolipwa zaidi wanapokea mishahara kuanzia Ksh50,00-60,000 kwa mwezi sawa na Tsh700,000-990,000 kwa mwezi.

Lakini je, uhamisho huo unaonyesha fursa zinazoongezeka kwa soka la wanawake na ongezeko la utambuzi wa vipaji na uwezo wa wachezaji wa kike Kenya?

Doreen Nabwire 'Dodo' alicheza na kuhudumu kama nahodha wa Starlets. Alichezea FC Zwolle huko de Eredivisie Vrouwen kutoka 2010 hadi 2011 na kuwa mwanamke wa kwanza Mkenya kucheza soka la kulipwa Ulaya.

Tangu mwaka 2016, amekuwa akifanya kazi kama Afisa wa Maendeleo ya Soka ya Wanawake na Mkurugenzi katika FKF. Anasema, hatua hizi zinaashiria hatua nzuri katika taaluma ya wachezaji hawa.

"Hii ni hatua nzuri kwani wachezaji wengi ambao wanahamia mataifa mengine kuwakilisha taifa letu. Hapo awali, hali hii haikuwa ya kawaida, lakini inaonyesha tuko sawa. ligi yetu imekuwa na ukuaji mkubwa hasa katika ligi Daraja la Pili (NSL) na la FKF-WPL kwa kuwa na timu zenye ushindani wa hali ya juu. Hatua ya wachezaji wenye vipaji kuondoka inaiimarisha na kuwaweka wazi wachezaji kwenye mapya kuendeleza talanta zao. Hii itafaidisha timu yetu ya taifa pia,” alisema Nabwire.

“Ligi ya Tanzania imevutia wawekezaji ambao wamewekeza kwa kiasi kikubwa tofauti na ligi yetu, tofauti na misukosuko inayokabili vilabu vya hapa nchini. Hata hivyo, juhudi zinaendelea ili kupata wadhamini na kuimarisha ukuaji wa ligi yetu. Tunapoendelea kufanya kazi kuelekea uboreshaji, kuna matumaini kwamba ligi itavutia uungwaji mkono unaohitajika ili kustawi katika siku za usoni," aliongeza Nambire.

Novemba mwaka jana, alipandishwa cheo hadi nafasi ya Mkuu wa Ligi na Mashindano katika FKF.

Fainali za michuano ya Cecafa 2019 zilizofanyika Tanzania Novemba 25, 2019, zilileta masikitiko kwa timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars na kocha wao mkuu, Bakari Shime.

Starlets iliifunga Tanzania mabao 2-0 na kutwaa ubingwa wa cecafa Women Championships jijini Dar es Salaam, Tanzania baada ya kushinda mechi zote bila kufungwa.

Kupoteza kwa Starlets bado kunabaki katika kumbukumbu ya Shime.

"Kenya imedhihirisha ni bora kuliko sisi tangu zamani. Kushindwa kwetu na Kenya katika michuano ya 2019 sitasahau lakini hatuwezi tukajilaumu. Tangu wakati huo, nchi yetu imewekeza katika soka kuanzia ngazi ya chini hadi taifa. Tulijifunza haya yote kutoka kwa Kenya ambao walianza soka la wanawake mapema kuliko sisi," alisema Shime.

Miaka minne baadaye, Shime ameiongoza Stars kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024 Morocco baada ya kukosekana kwa miaka 14.

 Stars ndiyo wawakilishi pekee kutoka Ukanda a Afrika Mashariki watakaoshiriki Wafcon. Wakati timu yao ya taifa ya wanaume, Taifa Stars, kwa sasa inawakilisha ukanda wa Afrika Mashariki katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) inayoendelea Ivory Coast.

Kocha wa zamani wa Starlets, David Ouma ambaye kwa sasa yuko na Coastal union inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanaume Tanzania, alichangia pakubwa katika kukuza soka la wanawake na alikuwa na timu ya taifa kwa miaka saba.

Ouma alijiunga na Coastal Union Novemba mwaka jana, kutoka Ligi Kuu ya FKF-PL akiwa Sofapaka FC.

Aliiongoza Starlets kunyakua taji la Cecafa 2019 na kuiongoza timu hiyo kufuzu kwa Wafcon kwa mara ya kwanza katika historia mnamo 2016.

"Kusema kweli nilijitolea 2014 - 2021 na mwishowe nilinawa mkono na nikajiondoa kwenye soka la wanawake baada ya kuacha alama kubwa ya kufuzu Wafcon na kushinda Cecafa, je, hii si historia ya kutosha kutoka kwangu? Yote haya yalifanyika ingawa hatukupata sapoti sana wakati huo,” alisema Ouma.

Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Yanga na Mkurugenzi wa sasa wa Masuala ya Sheria, Uzingatiaji na Utawala, Simon Patrick asisitiza haja ya mechi kurushwa kwenye runinga bila kuacha za wanawake.

"Bila hivyo, michezo ingetatizika kuwafikia na kuwashirikisha mashabiki wao, huku watangazaji wakikosa maudhui ya kuvutia wanayohitaji ili kuvutia watazamaji. Utangazaji huruhusu mashabiki kote ulimwenguni kutazama timu wanazozipenda bila kujali mahali zilipo. Pia hutoa jukwaa kwa wadhamini na watangazaji kufikia hadhira kubwa na kuifanya kuwa sehemu muhimu ya tasnia ya michezo,” alisema Patrick.

Patrick aliongeza; "Michezo ni ajira. Biashara ya soka  Tanzania husaidia kuuza wachezaji kwa klabu za nje kupitia maskauti, kuuza jezi na hivyo ndivyo Simba na Yanga wamefanikiwa katika kuuza kazi yao Tanzania."

Lakini je, Wakenya wanapenda sana ligi ya ndani, Patrick alikuwa na haya ya kusema;

"Kenya, wafuasi wengi wa soka wanapenda sana Ligi Kuu England (EPL) ikilinganishwa na ligi ya ndani. Hii ni tofauti na hali ya Tanzania, mashabiki wanaonyesha shauku kubwa kwa ligi yao ya nyumbani."

Kutumia vizuri mitandao ya kijamii, timu nyingi za soka na hata wachezaji kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii kama TikTok na Instagram wanaweza kuvutia wafadhili zaidi.

Alex Alumirah ambaye ni kocha wa zamani wa Starlets na kwa sasa ni Mkuu wa Maendeleo ya Soka katika Fountain Gates Princess anasema uwepo wa klabu ya soka kwenye mitandao ya kijamii inaweza kusababisha mauzo ya bidhaa kuongezeka.

“Wachezaji watambue mitandao ya kijamii inaweza kuwauza kutokana na kile wanachoweka. Unapata wachezaji wa soka hawatumii majina halisi kwenye mitandao ya kijamii, mfano golikipa anaweza kutumia jina kama, ‘Sishiki Nduki Moto’ au ‘Hitilafu Kelele ya Kayole’ maudhui yanachanganya. Weka mitandao yako ya kijamii kuwa safi haswa ikiwa unatumia jina lako halisi," alisema Alumirah.

Kwa mfano, Aquino ana wafuasi 111,000 kwenye Facebook, 45,300 kwenye tiktok na 74,200 kwenye Instagram, na hivyo kumfanya kuwa mwanasoka wa kike anayefuatiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii nchini Kenya na Tanzania.

“Lazima ujifunze kutengeneza maudhui kulingana na unachofanya, acha kukurupuka kutoka mada moja hadi nyingine, mwaka jana katika viwango vya mtandao wa kijamii wa Fifa Tanzania ilishika nafasi ya tatu kati ya klabu tano bora za Afrika, Simba, Yanga na Fountain Gates waliongoza," aliongeza Alumirah.

Ligi ya Tanzania imesifiwa kwa ubora wake, lakini ni wachezaji wachache waliohamia nje ya nchi kwa nafasi nzuri licha ya uwezo wa ligi hiyo.

Washambuliaji Topister Situma, aliyekuwa Simba, sasa anachezea Sirina Grevenon ya Ugiriki, wakati Shilwatso alijiunga na FC Kryvbas Women ya Ukraine zote kutoka Singida Fountain Gates

Beki Dorcas Nashivanda alirejea nyumbani kujiunga tena na timu ya FKF-WPL Zetech Sparks.

Kwa sasa tuna wanasoka 15 wa kike wanaocheza soka la kulipwa Tanzania ikiwa na wachezaji walioko Simba (5), Fountain Gates Princess (2), Yanga (3) na Bunda Queens (5).


Fountain Gates Princess:

Monocah Sedah

Inviolata Mukosh


Simba Queens:

Corazone Aquino

Elizabeth Wambui

Caroline Rufaa

Jentrix Shikangwa

Ruth Ingotsi


Yanga Princess:

Wincate Kaari

Janet Moraa Bundi

Airin Madalina


Bunda Queens:

Saumu Baya

Liz Khisa

Fanis Kwamboka

Eunice Kwangu

Lorine Awuor