Voliboli yapewa kipaumbele Mombasa
SERIKALI Kaunti ya Mombasa imeahidi kuimarisha mchezo wa voliboli kwa kuhakikisha unapata umaarufu kama ilivyo michezo mingne.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Wizara ya Vijana, Michezo, Jinsia na Huduma za Jamii, Khamis Juma Kurichwa, aliyesisitiza serikali ya kaunti hiyo iko na mikakati kabambe inayolenga kuboresha voliboli kutumika kama kigezo cha ajira kwa vijana.
Kurichwa alitaja baadhi ya mikakati hiyo ni kuhakikisha kunapatikana viwanja bora pamoja na kutoa usaidizi wa vifaa hitajika kama vile neti, mipira na sare.
Katibu huyo alisema chini ya uongozi wa Gavana Abdulswamad Nassir, wako tayari kuketi na wadau wa mchezo huo ili kuona ni mbinu gani wanazofaa kuzitumia ili kuboresha mchezo huo. Alisema mchezo huo ni miongoni mwa iliyosahaulika hali inayowanyima fursa vijana wenye vipaji kuviendeleza.
“Mara nyingi voliboli utaushuhudia ukifanyika kwenye mashindano ya shule za msingi na zile za upili kisha kusaulika hivyo napenda kuwahakikishia wachezaji pamoja na wadau wa mchezo huo kwamba Serikali Kaunti ya Mombasa iko tayari kuimarisha mchezo huo,” alisema.
Kurichwa alitoa hakikisho hilo alipokuwa eneo la Mtongwe Likoni kujionea mashindano ya voliboli yaliyojumuisha timu 12 ambapo nne zilikuwa za wanawake na nane za wanaume.
Mwenyekiti wa voliboli Pwani Kusini, Benjamen Choge, aliiomba serikali ya kaunti kuwashika mkono ili kuboresha mchezo huo.