Ukarabati Uwanja Moi Kasarani kukamilika Aprili

Muktasari:
- Uwanja huu ni sehemu ya viwanja vitakavyotumika kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024, ambayo imesogezwa mbele hadi Agosti 2 mwaka huu, na pia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Serikali ya Kenya inatarajia kumaliza ukarabati wa Uwanja wa Moi Kasarani mwezi Aprili. Uwanja huu wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 ulianza kufanyiwa ukarabati tangu Desemba 2023.
Uwanja huu ni sehemu ya viwanja vitakavyotumika kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024, ambayo imesogezwa mbele hadi Agosti 2 mwaka huu, na pia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Kenya itakuwa mwenyeji wa michuano ya CHAN 2024 na AFCON 2027 pamoja na nchi jirani za Uganda na Tanzania.
Akizungumza baada ya kukagua kazi za ukarabati zinazoendelea kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Katibu Mkuu wa Michezo wa Kenya, Peter Tum alisema kwamba mkandarasi wa mradi anatarajiwa kumalizia kazi ya awamu ya pili ya mradi huo kulingana na tarehe mpya.

“Ukarabati wa Moi Kasarani utakamilika kwa asilimia 100 mwezi Aprili. Awali, tulisitisha baadhi ya kazi katika awamu ya pili kwa sababu hatungependa iwe sehemu ya ujenzi wakati tunahitaji kuwa wenyeji wa CHAN 2024, lakini baada ya kusogezwa mbele kwa tarehe ya kuanza kwa michuano hii (hadi Agosti 2 hadi 28), tulirudisha shughuli zote zilizopangwa kwa awamu ya pili ya ukarabati. Hii inamaanisha kwamba mwezi Aprili, hapa hatutakuwa na ujenzi tena na utakuwa tayari kuandaa michuano yoyote,” aliongeza.
Awali, CHAN 2024 ilikuwa imepangwa kufanyika mwezi Septemba mwaka jana, kabla ya kuahirishwa hadi Februari 1-28 mwaka huu, na baadaye kusogezwa mbele hadi mwezi Agosti mwaka huu.
Wakati wa kuahirisha michuano hiyo, Rais wa CAF, Patrice Motsepe alisema Januari 15 kwamba Kenya, Uganda, na Tanzania zilihitaji muda zaidi ili kuhakikisha miundombinu yao inakidhi viwango vinavyohitajika na Shirikisho la Soka la Afrika.

Uwanja wa Nyayo ni uwanja mwingine ambao Kenya iliuteuwa kwa ajili ya michuano ya CHAN 2024, huku viwanja vya mazoezi vikiwa ni: MISC Kasarani Annex, Police Sacco Stadium, na Ulinzi Sports Complex.
Serikali ya Kenya ilishindwa kumaliza ukarabati wa Moi Kasarani ifikapo Desemba 2024. Uwekaji wa njia ya Tartan, uboreshaji wa jukwaa la vyombo vya habari, ufungaji wa mfumo wa sauti, na kumalizia ufungaji wa paa.
Awamu ya kwanza ya ukarabati ilihusisha ufungaji wa taa, viti, vyumba vya kubadilishia nguo na vyoo, pamoja na kubadilisha muonekano wa uwanja.

Nicholas Musonye, mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uongozi ya Kenya kwa michuano ya CHAN 2024 na AFCON 2027, na Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya, Hussein Mohammed ni baadhi ya maafisa waliokuwapo na Tum katika ziara ya ukaguzi.