Tusker yaianza msimu mpya kwa kipigo cha 2-0, kocha awa mbogo
Muktasari:
- Winga wa zamani wa Gor Mahia, Boniface Omondi, ndiye aliyekuwa shujaa wa KCB inayoongozwa na aliyekuwa kocha wa Tusker, Robert Matano, baada ya kufunga mabao yote mawili. Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 19 kwa kichwa akimalizia krosi ya December Kisakah.
Pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Soka ya Kenya (FKF) 2025/26 limefunguliwa rasmi, kwa mabingwa wa zamani Tusker FC, waliomaliza msimu uliopita katika nafasi ya nne, walianza kampeni kwa kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa KCB katika mechi pekee ya wiki ya kwanza iliyopigwa jana Ijumaa kwenye Uwanja wa Kasarani.
Winga wa zamani wa Gor Mahia, Boniface Omondi, ndiye aliyekuwa shujaa wa KCB inayoongozwa na aliyekuwa kocha wa Tusker, Robert Matano, baada ya kufunga mabao yote mawili. Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 19 kwa kichwa akimalizia krosi ya December Kisakah.
Wakati Tusker ikijipanga ili kusawazisha, mshambuliaji Eric Kapaito alipoteza nafasi mbili muhimu dakika ya 24 na 30. KCB iliongeza bao la pili kupitia Omondi aliyemalizia kwa urahisi na kuifanya timu hiyo kwenda mapumzikoni ikiwa mbele kwa 2-0.
Kipindi cha pili, Tusker ilipata nafasi ya kupunguza tofauti baada ya kupata penalti, lakini Kapaito alipiga juu ya lango na kuendeleza uongozi wa KCB.
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Tusker Charles Okere alikiri kikosi hicho hakikuwa bora vya kutosha kuibuka na alama.
“Ilikuwa mechi yetu ya kwanza msimu huu, na naamini ilikuwa ngumu, tulikuwa tunakutana na timu yenye nguvu pia, lakini tunawapongeza wapinzani kwa ushindi. Walifanya vya kutosha kushinda. Ni mechi ya kwanza, lakini naamini tulipaswa kufanya vizuri zaidi,” alisema Okere.
Kuhusu wachezaji wapya, Okere aliongeza:
“Ni wachezaji wazuri na naamini watazoea haraka falsafa na mbinu za timu. Tukiwapa muda zaidi wa mazoezi na mechi, watakuwa bora zaidi kwa sababu ni suala la mshikamano ndani ya kikosi. Lakini bado ni jambo tunalopaswa kulifanyia kazi kwa bidii.”
Akizungumzia makosa yaliyowagharimu, alieleza:
“Tulitengeneza nafasi kadhaa za kufunga ambazo hatukuzitumia. Tunapaswa kuboresha hilo kwa mechi zijazo. Ni lazima tuwe na makali ya kufunga. Tayari kuna presha na tunastahili kuzoea mapema ili tuweze kusalia katika mbio na wapinzani wetu.”
Kuhusu Kapaito aliyekosa penalti, Okere alisema:
“Kapaito ni mshambuliaji wa kiwango cha juu, anayeifungia timu mabao muhimu. Leo ilikuwa siku mbaya kwake tu, lakini katika mechi inayofuata akipata nafasi, ataendelea kupiga penalti na kufunga.”
Alimalizia kwa kusema:
“Hii ilikuwa mechi ya kwanza ambayo ni muhimu kama ya mwisho. Tulitaka pointi zote tatu, lakini kupoteza pointi hizi ni jambo tunalopaswa kurekebisha mapema ili tuwe katika nafasi nzuri ya kuwania taji.”
Kwa upandea wa
Matano asifu mwanzo mzuri wa KCB kwa uchezaji bora, akisema wachezaji walifuata maagizo yake kikamilifu.
“Tulikuwa na kujiamini na mshikamano bora kwa mechi hiyo na ndicho kilichoinua timu yangu. Aidha, azma na maandalizi yetu yalionekana uwanjani. Vijana walicheza vile nilivyotarajia. Tumekuwa pamoja kwa miezi miwili iliyopita na imetuletea matokeo haya,” alisema Matano.
Alipoulizwa kama anapania taji la ligi na KCB, Matano alijibu:
“Msimu ndio umeanza, safari bado ni ndefu. Tumeshacheza mechi moja na zimesalia 33. Tutazungumza tukiwa njiani, lakini mimi niko tayari.”
Ligi itaendelea tena leo Jumamosi kwa Kariobangi Sharks itakuwa wenyeji wa Bandari kwenye Uwanja wa Kasarani Annex, huku AFC Leopards ikikabiliana na Sofapaka kwenye Ulinzi Complex.