Tusker vs Kenya Police vita ya kileleni Ligi Kuu Kenya

Muktasari:
- Mechi hii ina umuhimu mkubwa kwani timu zote zinashikilia nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi na zina alama 37 kila moja, zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa. Kenya Police inaongoza kwa tofauti ya mabao ikifunga 24 na kuruhusu 10 wakati Tusker ikiwa nayo 31 na nyavu zao kutikiswa mara 22, zote zikicheza mechi 19.
WIKIENDI hii katika mchezo wa kutazamwa zaidi kwenye Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) utakuwa ni kati ya Tusker na Kenya Police, utakaochezwa Uwanja wa Kenyatta uliopo Machakos.
Mechi hii ina umuhimu mkubwa kwani timu zote zinashikilia nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi na zina alama 37 kila moja, zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa. Kenya Police inaongoza kwa tofauti ya mabao ikifunga 24 na kuruhusu 10 wakati Tusker ikiwa nayo 31 na nyavu zao kutikiswa mara 22, zote zikicheza mechi 19.
Mechi hii, itakayochezwa Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni, itakuwa na athari kubwa kwa timu yoyote itakayopoteza, kwani mshindi atapata alama tatu na kujiweka nafasi nzuri katika mbio za ubingwa.
Vile vile, mechi hii inazikutanisha timu yenye safu ya ushambuliaji bora zaidi dhidi ya timu yenye ulinzi imara zaidi.
Tusker inaongoza kwa kuwa na safu ya ushambuliaji bora zaidi, ikiwa imefunga mabao 31 na kuruhusu 22, huku Kenya Police ikiwa na ulinzi bora zaidi, ikiwa imefungwa mabao 10 pekee na kufunga 24.

Kocha wa Tusker, Charles Okere, ambaye alichukua mikoba kutoka kwa Robert Matano aliyetimkia Fountain Gate ya Ligi Kuu Tanzania Bara mwanzoni mwa msimu huu, amesema mechi hii itakuwa ngumu lakini lazima timu yake iwe na utulivu.
"Kila mchezo ni mgumu na tunajua hisia za mashabiki ni kubwa, lakini lazima tuwe watulivu. Jambo muhimu ni kuboresha kutoka kwenye mchezo uliopita ambao hatukuruhusu bao na lilikuwa ni moja ya malengo yetu," amesema Okere.
Tusker haijapoteza mechi yoyote kati ya nne zilizopita na imeonyesha kiwango kizuri dhidi ya wapinzani wake.
Mchezaji anayetajwa katika mafanikio ya timu hii ni mshambuliaji Ryan Ogam, mwenye umri wa miaka 20, ambaye anaongoza kwa mabao akiwa nayo 15, akimzidi sita anayemfuatia mshambuliaji wa KCB, Francis Kahiro.
Hata hivyo, Ogam anasema anachokijali kwa sasa ni mechi dhidi ya Kenya Police, baada ya mpango wake wa kuhamia klabu ya USM Alger ya Algeria kuvunjika mapema wiki hii.
“Mimi ni mchezaji wa Tusker FC na ninalenga kufanya vyema katika kila mchezo hadi mwisho wa msimu. Malengo yangu ni kufunga mabao zaidi," amesema Ogam ambaye msimu huu amejiwekea malengo ya kufunga mabao kati ya 25 na 30.
"Chochote kuhusu uhamisho wangu ni wa wawakilishi wangu na wazazi wangu," aliongeza Ogam, ambaye alijiunga na watengeneza bia, Rainbow FC mwanzoni mwa msimu huu.
Ogam atachuana vikali na safu ya ulinzi ya Kenya Police yenye watu kama Aboud Omar, Baraka Badi, Brian Okok na Daniel Sakari, ambao wanatajwa kuwa bora zaidi kwenye ligi.
Kwa upande wa Kenya Police, ulinzi wao umeimarika zaidi, na Aboud Omar, Baraka Badi, Brian Okok, na Daniel Sakari wamekuwa nguzo muhimu.

Kenya Police pia imetoka kutoruhusu bao katika mechi 11 zilizopita, tangu Kocha Etienne Ndayiragije aanze kuinoa timu hiyo Novemba 29, 2024.
Timu hiyo imeimarisha safu ya ushambuliaji kwa kumtambulisha mshambuliaji Mohamed Bajaber kutoka Nairobi City Stars, ambaye ameongeza mabao matano msimu huu.
Mechi hii itakuwa ya kuvutia na ina maana kubwa kwa timu zote zinazoshindania nafasi za juu katika ligi.
Katika mechi saba kati ya Tusker na Kenya Police, Tusker imeshinda mara tatu, Kenya Police mara moja, huku nyingine tatu zikimalizika kwa sare.
Wakati huohuo, kocha mpya wa Gor Mahia, Sinisa Mihic, atacheza mechi yake ya kwanza katika ligi ya Kenya leo Jumamosi, wakati timu yake itakapopambana na Mathare United kwenye Uwanja wa Dandora, Nairobi.
Mihic, mwenye umri wa miaka 48, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita hakuwa na timu anayoifundisha, hivyo ataiongoza Gor Mahia inayoshika nafasi ya tatu kwa alama 31, huku Mathare ikishika nafasi ya 14 kwa alama 21 zote zikicheza mechi 18.
Katika michezo mingine ya ligi hiyo wikiendi hii, AFC Leopards itaikaribisha Kariobangi Sharks wakati Shabana nayo ikiwa mwenyeji wa Posta Rangers.
RATIBA YA MICHEZO YA KPL WIKIENDI HII
LEO JUMAMOSI
Bidco United vs Nairobi City Stars (Kenyatta, Machakos, saa 7:00 mchana)
Bandari vs Sofapaka (Mbaraki, Mombasa, saa 9:00 alasiri)
Tusker vs Kenya Police (Kenyatta, Machakos, saa 10:00 jioni)
Mathare United vs Gor Mahia (Dandora, Nairobi, saa 10:00 alasiri)
KESHO JUMAPILI
Ulinzi Stars vs Kakamega Homeboyz (Dandora, Nairobi, saa 7:00 mchana)
KCB vs Murang’a Seal (Kenyatta, Machakos, saa 7:00 mchana)
Mara Sugar vs FC Talanta (Awendo, Migori, saa 9:00 alasiri)
Posta Rangers vs Shabana (Kenyatta, Machakos, saa 10:00 jioni)
AFC Leopards vs Kariobangi Sharks (Dandora, Nairobi, saa 10:00 jioni)