Straika Starlets apiga tano Rwanda
STRAIKA wa timu ya taifa ya wanawake, Harambee Starlets, Judith Atieno alifunga mabao matano mapema wiki hii na kuisaidia Rayon Sports Women kuizaba ES Mutunda mabao 10-0 katika nusu fainali mkondo wa kwanza Kombe la Amani la Rwanda kwa Wanawake iliyopigwa Uwanja wa Skolx jijini Kigali.
Licha ya kujiunga na timu hiyo kwenye mzunguko wa pili, Atieno ametupia kambani mabao 42 akiwa na asisti 19 katika michezo 19 na kumfanya kuwa mfungaji bora wa pili.
Siku ya Jumamosi, Rayon ilipandishwa daraja hadi Ligi Kuu ya Wanawake Rwanda Divisheni ya Kwanza baada ya kuwachapa mabao 10-1 Nasho FC huku Atieno akifunga mabao mawili na kusaidia mara mbili.
“Ninafuraha kwamba tulipandishwa daraja la juu. Kucheza katika Ligi Daraja la Pili haikuwa rahisi, lakini tulijitolea kwa uwezo wetu wote. Ninasubiria kucheza katika daraja la juu msimu ujao na kufunga mabao zaidi,” alisema.
Akizungumza na MWANASPOTI, Katibu Mkuu wa Rayon Sports, Patrick Namenye, alisema anafurahi kuona timu hiyo imeichukua msimu mmoja tu kupanda hadi daraja la kwanza.
Alisema wapo mbioni kutwaa ubingwa wa ligi na wamebakiza mchezo mmoja kutinga fainali ya Kombe la Amani.
Atieno ambaye alijiunga na Rayon Sports akitokea Mathare United Women inayoshiriki Ligi ya Taifa, pia yuko kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Machi akipambana na Mukeshimana Dorothee na Imanizabayo Florence.