Sofapaka yaibomoa Kibera Black Stars

MABINGWA Ligi Kuu Kenya 2009, Sofapaka FC, wamemteua Paul Ogai aliyekuwa akiifundisha Kibera Black Stars kuwa kocha msaidizi.
Taarifa ya Sofapaka kwenye mtandao wa kijamii ilidhibitisha kumnasa Ogai atakayesaidiana na kocha mkuu, David Ouma.
“Tunafuraha kutangaza tumepata huduma za kocha Paul Ogai kutoka Kibera Black Stars. Ogai anajiunga na klabu kuwa naibu wa kocha mkuu David Ouma,” ilisema taarifa ya Batoto Ba Mungu.

Klabu hiyo ipo kwenye mchakato wa kusaka mfadhili mpya baada ya kuachana na mfadhili wao wa awali ambayo ilikua kampuni ya kubeti huku pia ikiondokewa na wachezaji nyota kama vile Lawrence Juma, Fredrick Odhiambo, Tsuma Said na Rody Manga.

Kocha msaidizi mpya wa Sofapaka mbali na Kibera Black Stars ashawahi kuzinoa baadhi ya timu za NSL kama vile Western Stima, Kisumu All Stars, Coast Stima na Palos FC.

Akiwa na Batoto Ba Mungu, Ogai anachukua nafasi ya Hillary Echesa ambaye alishikilia wadhifa huo kwa muda baada ya Ouma kufanywa kaimu kocha kufuatia kutimuliwa kwa Ken Odhiambo Februari mwaka huu.

Ouma aliyethibitishwa mkufunzi wa Sofapaka Juni mwaka huu, ameiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya nane FKFPL msimu uliopita.