Riadha Kilifi yapiga mkwara

Muktasari:

  • KILIFI. KAUNTI ya Kilifi imepania kuhakikisha inasitisha utawala wa Kaunti ya Taita Taveta katika mashindano ya Mbio za Nyika za Jimbo la Pwani zitakazofanyika Kwale mwishoni mwa wiki hii.

KILIFI. KAUNTI ya Kilifi imepania kuhakikisha inasitisha utawala wa Kaunti ya Taita Taveta katika mashindano ya Mbio za Nyika za Jimbo la Pwani zitakazofanyika Kwale mwishoni mwa wiki hii.
Akiongea baada ya kukamilika kwa Mbio za Nyika za Kaunti ya Kilifi, Katibu wa Chama cha Riadha cha Kenya (AK) tawi dogo la Kilifi, Felix Ngala, alisema wamechagua kikosi cha wanariadha 42 mahiri watakaopigania kushinda mashindano hayo.
“Tunawaambia wapinzani wetu wawe tayari kwani raundi hii, tumejiandaa vizuri na tuna kikosi imara ambacho kitafanya kazi ya kumaliza utawala wa Taita Taveta kushinda mbio hizo,” alisema Ngala.
Katika mbio hizo za Kaunti ya Kilifi, rekodi mpya tatu ziliwekwa kwenye vitengo vya wavulana wa umri chini ya miaka 20 za kilomita nane, wanaume wakubwa za kilomita 10 na za mchanganyiko za relay.
Isaiah Wanje wa Malindi aliweka rekodi mpya ya wavulana wa umri chini ya miaka 20 akikimbia kwa dakika 33 nukta nane akivunjilia mbali rekodi ya awali ya dakika 36:6 ya Brian Nzai.
Rekodi nyingine iliwekwa na Teddy Mwaringa wa Malindi aliyeivunja rekodi ya zamani ya Erick Okoth ya dakika 35:4 alipotumia dakika 34:3.
Wakimbiaji Dismas Mwalimu, Ibrahim Tembo, Christine Kalume na Sanita Mweni waliweka rekodi mpya ya Mixed Relay wakitumia muda wa dakika 27:5 na kuvunja rekodi ya awali ya dakika 27:8 iliyowekwa mwaka jana na Martin Ngala, Rama Wilson, Beatrice Dhahabu na Gladys Sanita.