Rais FKF kizimbani

JAJI Esther Maina amesema hana mamlaka kisheria kumzuia Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma kumfungilia kesi Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nick Mwendwa, ambaye kwa siku za hivi karibuni alidai yuko huru baada ya kesi zilizokuwa zinamkabili kufutwa.
Mwendwa atasimama kizimbani Jumatatu katika Mahakama ya Kiambu baada ya Mahakama Kuu kukata kuzuia DPP kumshitaki upya.
Mwendwa alishitakiwa kwa tuhuma za kula njama kulaghai FKF zaidi ya Sh38 milioni na amekuwa akipambana mara kadhaa kusafisha jina lake baada ya Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohamed kuivunja shirikisho hilo Novemba 11 mwaka jana.
Kesi hiyo iliondolewa chini ya Kifungu cha 87 cha Kanuni ya Adhabu Julai 6 mwaka huu lakini siku moja baadaye, DPP alimfungulia mashtaka upya katika Mahakama ya Kiambu. Hata hivyo, Mwendwa alipata zuio kutoka Mahakama Kuu ikisitisha mashitaka yoyote mapya dhidi yake.