Police yaitia pingu Butali Warriors

WAFALME wa zamani wa magongo Ligi Kuu nchini, Kenya Police wamevunja rekodi ya Butali Warriors ya kutoshindwa msimu huu kwa kuizaba bao 1-0 ugani City Park, Nairobi katika mechi ya kutamatisha kampeni za ligi kuu msimu huu.

Butali chini ya kocha, Zack Aura, ilikuwa imecheza mechi 17 bila kupoteza lakini ilishindwa kutimiza azma ya kumaliza msimu ‘unbeaten’ katika mechi ambayo pande zote zilionyesha mchezo safi.

Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa kwa njia ya penalti na Sammy Oungo baada ya Titus Kimutai kuchezewa visivyo katika eneo hatari.

Hata hivyo dakika ya 48 Butali Warriors nayo ilipata penalti lakini kipa wa Police, Joshua Omondi, alikua imara kunusuru baio.

“Nashukuru wachezaji wangu wote kwa kufanya kazi nzuri kumaliza nafasi ya pili pia kujikatia tiketi ya moja kwa moja kushiriki ngarambe ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huu,” alisema kocha wa Kenya Police, Patrick Mugambi.

Nao malkia wapya wa mchezo huo, Scorpions ya Chuo Kikuu Cha Strathmore iliipiga DFG Wolverines mabao 2-0 kwenye mechi ya mwisho kitengo hicho.