Pacome, Duke Abuya mbabe kujulikana Alassane Ouattara
Muktasari:
- Timu hizo mbili zitakutana kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara jijini Abidjan, katika mechi ya mwisho ya Kundi F, kesho Jumanne Oktoba 14, 2025 saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, ilifanya mazoezi yao ya kwanza nchini Ivory Coast jana Jumapili jioni Oktoba 12, 2025, ikiwa ni maandalizi ya mechi ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026 dhidi ya wenyeji wao, Ivory Coast, The Elephants.
Timu hizo mbili zitakutana kwenye Uwanja wa Alassane Ouattara jijini Abidjan, katika mechi ya mwisho ya Kundi F, kesho Jumanne Oktoba 14, 2025 saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Harambee Stars inatarajiwa kufanya mazoezi yao ya pili leo Jumatatu Oktoba 13, 2025 kwenye uwanja huo wa mechi kabla ya kumaliza kampeni yao ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026.
Kenya itaingia uwanjani kwa lengo la kuvunja rekodi ya wenyeji Ivory Coast, ambayo inahitaji ushindi ili kujihakikishia tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika mwaka 2026 nchini Canada, Mexico na Marekani.
Ivory Coast hadi sasa haijapoteza wala kuruhusu bao katika hatua hii ya kufuzu na inaongoza kundi ikiwa na pointi 23, moja zaidi ya Gabon iliyoko nafasi ya pili, ambayo itaikaribisha Burundi kesho Jumanne mjini Franceville. Ivory Coast inahitaji ushindi ili kujihakikishia kumaliza kinara bila ya kuangalia matokeo ya Gabon.
Kocha wa Harambee Stars, Benni McCarthy, amesisitiza hadharani kuwa Kenya haitakuwa rahisi kwa Ivory Coast, jambo linalotarajiwa kufanya mchezo huo kuwa wa kuvutia.
Kwa sasa Harambee Stars inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 12, mbili zaidi ya Gambia na Burundi zenye pointi 10 kila moja, zikitofautiana kwa tofauti ya mabao. Seychelles inaburuza mkia bila pointi.
Mshambuliaji Ryan Ogam wa Harambee Stars, alifunga bao dhidi ya Burundi katika mechi ya kufuzu iliyofanyika Oktoba 9, 2025, kwenye Uwanja wa Intwari jijini Bujumbura.
Msafara wa Harambee Stars uliwasili Abidjan Jumamosi jioni Oktoba 11, 2025 na kuelekea moja kwa moja kwenye hoteli iliyoko eneo la Akouedo, takribani kilomita 30 kutoka Uwanja wa Alassane Ouattara.
Mjumbe wa NEC wa FKF, Dan Shikanda, ambaye alisafiri na timu, amesema wachezaji wako katika hali nzuri ya kisaikolojia na kimwili.
“Walifanya mazoezi ya kurejesha nguvu Jumapili asubuhi, yaliyohusisha kunyoosha misuli kwa muda wa saa mbili na kuogelea kwa ajili ya kupumzisha miili,” amesema Shikanda, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Harambee Satrs.
Ameongeza kuwa kikosi hicho hakikuathiriwa na maandamano ya kabla ya uchaguzi yaliyotokea katika eneo la Cocody jijini Abidjan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la kimataifa AP, polisi wa Ivory Coast waliwakamata watu 237 kufuatia vurugu hizo zilizotokea Jumamosi. Eneo la Cocody liko umbali wa kilomita nne tu kutoka hotelini walipofikia Harambee Stars.
Shikanda amesema pia Harambee Stars imefanya mazoezi yao ya kwanza katika Shule ya Lycée Classique Cocody, ambayo iko ndani ya eneo lililokuwa limeathiriwa na maandamano hayo.
Athanas Oballa, Mkuu wa Miradi Maalum na Timu za Taifa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF), amesema kupitia mahojiano na Nation Sport kwamba wako katika mawasiliano na Ubalozi wa Kenya nchini Ivory Coast kuhakikisha usalama wa timu.
“Tunafahamu kuhusu maandamano hayo na tumekuwa tukichukua tahadhari zote muhimu kwa kushirikiana na ubalozi wa Kenya. Kwa sasa eneo tunaloishi Abidjan ni tulivu,” amesema Oballa.
Ameongeza kuwa timu ilipata nafasi ya kufanya chakula cha mchana na Balozi wa Kenya nchini Ivory Coast, Christopher Langat, kama ishara ya kuwatakia mafanikio kabla ya mchezo huo muhimu.