Oyoo aitwa fasta kuokoa jahazi

ALIYEKUWA kocha wa Thika Queens na Mombasa Olympic, Joseph Oyoo, amejiunga na Fortune Ladies inayoshiriki Ligi ya Taifa Wanawake Daraja la Kwanza.

Akidhibitisha uteuzi huo, meneja wa Fortune Ladies, Samuel Sanya Hamala, alisema ujio wa kocha Oyoo utaboresha zaidi hali ya kikosi chake.

“Oyoo ni kocha mwenye uzoefu na ujio wake ni kama baraka kwa Fortune inapopambana kupiga hatua katika ligi,” alisema Hamala.

Kocha huyu alionekana na timu hii katika ufuo wa Jomo Kenyatta Public Beach wakijifua kwa mechi dhidi ya Kahawa Queens ya FKF Women Cup itakayopigwa uwanja wa Ronald Ngala Primary, Jumamosi.

Mkufunzi huyu ni kati ya waanzilishi wa soka la akina dada jimbo la Pwani akianza kuvuma miaka ya 90 na timu ya Mombasa Railways, Shule ya Upili St John’s ya Kaloleni, Kilifi na baadaye Mombasa Olympic.

Oyoo aliagana na Thika Queens mwanzoni mwa mwezi uliopita kutokana na kubanwa na shughuli za kifamilia.

Fortune Ladies imekuwa vuguvugu katika michuano yake ya ligi matokeo ambayo yamechangiwa na ukosefu wa ufadhili na kocha aliyehitimu barabara.

Aidha, Hamala amesema licha ya pandashuka za ufadhili, wataendelea kupambana kufa na kupona kuhakikisha wamefikia malengo yao