OLUNGA AJITOA NGORI KIWANGO STARS

NAHODHA wa Harambee Stars, Michael Olunga kajitoa kwenye ngori ya lawama kuhusu kiwango chake anapokuwa na timu ya taifa, ikilinganishwa na pale anapoichezea klabu yake.
Olunga amekuwa kwenye fomu ya kutisha katika klabu zote alizochezea. Msimu huu, ameendelea kuwabamba mashabiki wa klabu yake ya Alduhail kule Qatar kutokana na makali yake mbele ya lango.
Toka msimu mpya wa ligi ya Qatar ulipoanza, Olunga  tayari amecheza mechi mbili na kufanikiwa kufunga magoli saba. kwa mabao hayo, Olunga sasa anaongoza jedwali la wafungaji.
Kiwango hicho kimeshindwa kuonekana kwenye mechi zake akiwa na Stars. Kwenye michuano za kufuzu kwa kombe la dunia 2022, mpaka sasa Stars wamecheza mechi nne na Olunga akacheza katika kila ya mechi hizo, tena kwa dakika zote tisini za kila mchezo.
Lakini pamoja na hilo, amefanikiwa kupachika bao moja pekee ikiwa ni kwenye sare ya 1-1 waliyostajili Stars dhidi ya Rwanda ugenini.
Sasa mashabiki na wachanganuzi wa soka wameanza kumchakachua na kuchanganua mchango wapo anapokuwa na timu ya taifa.
Ila Olunga karuka ngori hiyo kwa kusisitiza kuwa kuichezea timu ya taifa ni tofauti kabisa na anapokuwa akiitumikia klabu hivyo hazipaswi kuchanganywa.
"Kumbuka hizi ni timu mbili tofauti. Kuichezea timu ya taifa ni tofauti kabisa na klabu. Mipango kazi na mikakati huwa ni tofauti kabisa baina ya kikosi cha taifa na klabu." Olunga anasema.
Tayari ndoto ya Stars kufuzu kwa kombe la dunia imefifia baada ya kulimwa ugenini na vile vile  nyumbani na Mali.
Wanakamata nafasi ya tatu kwenye kundi E nyuma ya Uganda na vinara Mali.