Okumu kulipa madeni Chemelil Sugar

MAMILIONI ya pesa yaliyotokana na uhamisho wa beki kisiki wa Harambee Stars, Joseph Okumu, yatatumiwa kulipa madeni ya wachezaji wa zamani wa Chemelil Sugar.


Haya ndiyo mapendekezo ya meneja timu wa zamani wa Chemelil Sugar, Hillary Ouma. Klabu ya Chemelil Sugar ilivunjwa  Novemba 2020 baada ya uwepo wake wa miaka 24.


Mapema wiki hii, Okumu aliyeichezea Chemelil kwa miaka miwili, alijiunga na K.A.A Gents inayoshiriki ligi kuu ya Ubelgiji akitokea IF Elsborg kwenye dili la uhamisho lililoghramu Sh449 milioni.
Kwa mujibu wa kanuni za uhamisho, klabu zote alizochezea Okumu alipokuwa na umri wa kati ya miaka  12 hadi 23,  hufidiwa na kiasi cha fedha kutoka kwa uhamisho huo ifahamikayo kama Solidarity fee.


Solidarity fee huwa ni asilimia 5% ya jumla ya fedha zilizotumika kwenye uhamisho wa mchezaji na hutumwa kwenye klabu zote pamoja na akademi alizozichezea katika umri huo wa 12-23.


Kutokana na uhamisho wa Okumu, klabu tano zitaifaidi fedha hizo ikiwemo Chemelil iliyovunjwa baada ya kukosa fedha za kuendesha klabu na pia kujiondoa kwa mfadhili wao mkuu.
Kutokana na uhamisho huo, Chemelil inakadiriwa itapokea Sh4.49 milioni klabu aliyoichezea kwa miaka miwili.
Hata hivyo kumekuwepo na mjadala kuhusu ni nani atakayepokea fedha hizo hasa ikizinmgatiwa kuwa klabu hiyo haipo tena baada ya kuvunjwa.


"Shirikisho inapaswa kutoa mwelekeo ni wapi fedha hizo zinapotakiwa kwenda kwa sababu klabu ilishavunjwa. Ila jambo la busara la kufanya na fedha hizo ni kuwalipa wachezaji wake wa zamani malimbikizi ya madeni yao. Kipindi uamuzi wa kuivunja klabu hiyo ulipoafikiwa, wachezaji hawakuwa wamelipwa mishahara yao kwa miezi zaidi ya mitano. Itakuwa haki kutumia fedha hizo kuwafidia sababu ya mchango walioutoa," Ouma kasisitiza.
Huku hayo yakijiri, klabu yake mpya K.A.A Gents imesema itamshirikisha Okumu mwenye miaka 236, na nahodha Mcameroon Michael Ngadeu Ngadjui kwenye safu yao ya kati.
"Joseph ni beki wa kati wa uhakika ambaye atatuongezea ubora kwenye kikosi chetu. Ni mrefu na udhibiti wake wa mipira ya hewani ni mzuri sana. Lakini pia ni mzuri sana kwenye utoaji wa pasi za kwenda mbele na ndio sababu klabu nyingi zilikuwa zikimwinda. Tunashukuru alichagua kujiunga nasi," kasema Meneja timu wa Gents, Tim Matthys.