Okoth wa Mathare aiumiza Shabana
Muktasari:
- Wakati huo huo, Gor Mahia iliivunja rekodi ya kutofungwa ya Posta Rangers msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye mechi iliyochezwa Uwanja wa Nyayo, Nairobi.
Mshambuliaji wa Mathare United, Dennis Okoth, aliiumiza timu yake ya zamani Shabana FC baada ya kufunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Soka Kenya (FKF Premier League) iliyochezwa jana Jumapili Oktoba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Gusii.
Wakati huo huo, Gor Mahia iliivunja rekodi ya kutofungwa ya Posta Rangers msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye mechi iliyochezwa Uwanja wa Nyayo, Nairobi.
Okoth, ambaye alichezea Shabana msimu uliopita kabla ya kujiunga na Mathare msimu huu, aliifunga timu yake ya zamani dakika ya 39 baada ya kipa Maxwell Mulili kushindwa kudhibiti mpira wake. Mathare iliongoza 1-0 hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilipoanza, kocha wa Mathare, John Kamau alimpumzisha Steve Kimari na kumuingiza Sammy Imbuye, huku kocha wa Shabana Peter Okidi akifanya mabadiliko mawili akiwaingiza Victor Otieno na Junior Munika kuchukua nafasi za Justine Omwando na Derrick Otieno.
Mabadiliko hayo yaliipa Shabana uhai katika safu ya ushambuliaji, lakini vijana wa Mathare “Slum Boys” walionyesha uimara na kujihakikishia pointi tatu baada ya filimbi ya mwisho.
Kocha Kamau amesifu wachezaji wake kwa kuonesha uthabiti akisema: “Nimefurahishwa na ushindi huu. Wachezaji wangu walionesha tabia na nguvu ya kupambana. Ilikuwa mechi ya vipindi viwili tofauti, tulitawala kipindi cha kwanza, wao wakatawala cha pili, lakini nimefurahi tumeshikilia hadi mwisho.”