Kocha Tusker aomba utulivu, aahidi kufanya makubwa
Muktasari:
- Tusker iliingia kwenye mchezo huo ikiwa imeshacheza mechi tatu ikipoteza mbili na sare moja. Ilianza ligi kwa kipigo cha 2-0 dhidi ya KCB, kisha ikafungwa 2-1 na Posta Rangers, mechi ya tatu ikaambulia alama moja baada ya kutoka 0-0 na Mathare United.
Kocha mkuu wa Tusker FC, Charles Okere, ameomba mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu baada ya kuwa na mwanzo mbaya kwenye Ligi Kuu ya Kenya, kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Shabana FC kwenye Uwanja wa Kasarani, Oktoba 5, 2025.
Tusker iliingia kwenye mchezo huo ikiwa imeshacheza mechi tatu ikipoteza mbili na sare moja. Ilianza ligi kwa kipigo cha 2-0 dhidi ya KCB, kisha ikafungwa 2-1 na Posta Rangers, mechi ya tatu ikaambulia alama moja baada ya kutoka 0-0 na Mathare United.
Katika mechi dhidi ya Shabana, Tusker ilijikuta ikiwa nyuma dakika ya 19 baada ya Austin Odongo kufunga bao baada ya kipa wa Tusker kushindwa kudaka mpira. Shabana ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Hata hivyo, kuingizwa kwa Ian Simiyu kuliibua matumaini kwa Tusker. Dakika tano tu baada ya kuingia, Simiyu alifunga bao la kusawazisha baada ya kumpokonya mpira beki Mark Okolla na kumalizia vyema wavuni. Bao hilo lilikuwa matokeo ya mashambulizi ya muda mrefu kutoka kwa Tusker iliyokuwa ikipiga kambi kwenye eneo la Shabana.
Katika kipindi cha pili, Tusker ilipoteza nafasi kadhaa kupitia Issa Lumumba na Dennis Iguma, huku krosi mbili za Omolle zikipita mbele ya lango la Shabana bila kuguswa.
Okere, ambaye amekuwa chini ya presha kutokana na matokeo mabaya, amewataka mashabiki wa Tusker wawe na uvumilivu akiahidi kurejesha uhai wa kikosi hicho.
“Tulitaka pointi tatu, lakini kupata pointi moja pia siyo matokeo mabaya ukizingatia bado tupo kwenye hatua za awali za msimu. Kwa mashabiki, naomba uvumilivu, kila kitu kitakuwa sawa. Tunapitia kipindi kigumu lakini hakitadumu,” amesema Okere.
“Tumeanza kupata muunganiko mzuri wa mchezo wetu, na ninataka kuwahakikishia mashabiki kwamba tukipata uthabiti, tutakwenda mbali. Bado tupo kwenye mbio za ubingwa, na tutapigana hadi mwisho.”
Akizungumzia bao la Simiyu, amesema: “Nilijua atafunga nilipomuingiza. Ni mchezaji ambaye ameonyesha maendeleo makubwa tangu ajiunge na Tusker, anafuata maagizo, na ametuokoa kwa bao hilo muhimu. Limepunguza presha kwa timu.
“Tumepunguza shinikizo kidogo, lakini bado hatujaridhika. Tunahitaji kujitahidi zaidi kuacha kufungwa. Tulifanikiwa kutoruhusu bao dhidi ya Mathare United, lakini leo tumefungwa, kwa hiyo lazima tuboreshe safu ya ulinzi, huku tukiboresha pia mashambulizi ili tufunge mabao mengi zaidi na kupata pointi tatu.
“Mechi za Tusker zote ni ngumu, kila mchezo ni kama fainali. Tunataka kuchukua kila mchezo mmoja baada ya mwingine, lakini jambo moja, najua tupo kwenye njia sahihi na mambo yatakuwa chanya hivi karibuni.”
Sare hiyo imeiacha Tusker katika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi kati ya timu 18, ikiwa na pointi mbili, nafasi moja tu juu ya eneo la kushuka daraja. Klabu hiyo ni ya pili kwa mafanikio nchini Kenya ikiwa na mataji 13 ya Ligi Kuu.
Kwa upande wa Kocha wa Shabana, Peter Okidi, ameonyesha kukerwa na matokeo hayo, akisisitiza kuwa timu yake ilistahili ushindi. Pia alikiri kuwa kuondolewa kwa mshambuliaji Brian Michira kutokana na majeraha kulivuruga mpango wao wa mchezo.
“Tulicheza vizuri kipindi cha kwanza na tulitawala mchezo, lakini kipindi cha pili tukaruhusu Tusker kuingia kwenye mchezo, jambo lililotuweka chini ya shinikizo,” amesema Okidi kwa Flashscore.
“Tulikuwa tumekuja hapa kwa lengo la kupata pointi tatu. Tumepoteza pointi ambazo hatukutegemea kupoteza, hasa tukiwa mbele kwa bao. Tutalazimika kurekebisha makosa yetu ya kuruhusu mabao rahisi.”
Kuhusu jeraha la Michira, Okidi amesema: “Alijeruhiwa mapema sana, tukalazimika kumtoa. Kuondoka kwake kuliathiri sana mpango wetu kwa sababu timu inamtegemea sana. Tulishindwa kucheza kwa mfumo tulioupanga.”
“Tunatumaini madaktari watamrejesha haraka, tunamhitaji akiwa fiti asilimia 100 ili atusaidie katika mbio za ubingwa.”
Akihitimisha, Okidi amesema: “Tulitaka kumaliza mapumziko ya kimataifa ya FIFA tukiwa na pointi tisa, lakini ni fedheha baada ya mchezo wa Tusker. Tulikuwa tumeshazipata pointi tisa tulipoongoza, lakini tukaziachia mikononi mwa Tusker. Tutatumia mapumziko haya kurekebisha mambo, na tukimrejesha Michira, tutaenda kutafuta pointi tulizopoteza.”
Licha ya sare hiyo, Shabana imesalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Kenya yenye timu 18, ikiwa na pointi saba.