Niliyosikia katika kikao cha Rihanna na Harmonize!

Kutoka kwenye fukwe za Barbados hadi Bongo, Rihanna anakutana na Harmonize na kufanya mazungumzo ya siri, wanajadili kuhusu muziki na biashara iliyopo ndani yake na namna gani ya kufikia mafanikio makubwa. 

Rihanna anampa Harmonize ushauri na mbinu za kivita ili kutengeneza himaya yake katika tasnia, Konde Boy anaandika yote katika shajara yake na kula kiapo cha utekelezaji kadiri ya uwezo wake.

Nikiwa kama mtu wa tatu katika kikao hicho, nilishuhudia na kusikia mazungumzo yao yote, leo ndugu yenu yamenifika kwenye koo, sina tena kifua cha kutunza siri hii, umri unaenda na uwezekano wa kusahau ni mkubwa, bora niwasimulie niliyosikia huko.

Basi Rihanna akamwambia Harmonize kama anataka kuwa msanii mkubwa asiwe mvivu wa kutoa albamu, wasanii wote wakubwa Tanzania, Afrika na duniani kwa ujumla wana utiriri wa albamu na ndio chemchem ya mafanikio kimuziki.

Mara moja nikarudisha kumbukumbu zangu nyuma kujua wasanii wenye albamu nyingi Tanzania ni kina nani, nikakuta ni Sugu na Lady Jaydee ambao ameacha alama kubwa katika Bongofleva, hivyo alichosema Rihanna ni sahihi.

Rihanna anasema alibaini hilo pindi alipoachia albamu yake ya tatu, Good Girl Gone Bad (2007), iliyojumuisha nyimbo kali kama Rehab, Hate That I Love You na Umbrella ambao ndio ulimpatia tuzo yake ya kwanza ya Grammy.

"Albamu hiyo ilipelekea nikachaguliwa kuwania vipengele saba katika tuzo za Grammy 2008 ila nikashinda kimoja cha Wimbo Bora wa Kushirikiana ambao ni Umbrella nikiwa na Jay-Z ambaye ndiye alinisaini Def Jam Recordings," Rihanna alimueleza Harmonize.

Ni albamu iliyouza nakala 162,000 katika wiki yake ya kwanza sokoni na hadi sasa imeuza milioni 2.8 kwa Marekani pekee, na ilishika nafasi ya pili chati za Billboard 200 ambazo ni maalamu kwa ajili ya albamu zinazofanya vizuri duniani.

Harmonize akamuuliza siri ya mafanikio ya albamu hiyo, Rihanna akajibu, 'upotenda zaidi, unapata nguvu ya kutenda zaidi', anasema ilimlazimu kutoa albamu mfululizo, yaani kila mwaka tena kwa ubora ule ule hadi alipoweza kufikia mafanikio hayo.

Utakumbuka Rihanna alianza kutoa albamu yake, Music of the Sun (2005), kisha ikafuata A Girl like Me (2006) na Good Girl Gone Bad (2007), ilikuwa miaka mitatu mfululizo ya kutoa albamu ndipo akapata Grammy yake ya kwanza.

"Kwa hapa Afrika kitu kama hicho nimekiona kwa Burna Boy wa Nigeria, nadhani ana moyo kama wangu, tunaweza kusema anaishi katika fikra zangu, unajua naye alitoa albamu mfulilizo kama mimi hadi aliposhinda Grammy?," alisema Rihanna.

Nikaingia mtandaoni kuangalia usahihi wa alichosema Rihanna, nikakuta baada ya Burna Boy kusaini Bad Habit/Atlantic Records na Warner Music Group, alitoa albamu tatu mfululizo ambazo ni Outside (2018), African Giant (2019) na Twice As Tall (2020).

Albamu hii ya tatu kuachia, Twice As Tall (2020) ambayo ni ya tano kwake kwa ujumla, ilishinda Grammy kama Albamu Bora ya Muziki Duniani ikiwa ni tuzo ya kwanza na ya pekee hadi sasa kwa Burna Boy, kwa hiyo Rihanna alikuwa sawa kumtolea mfano.

Rihanna akamwambia Harmonize baada ya kujifunza hilo, aliamua kutoa albamu nne mfululizo ambazo ni Rated R (2009), Loud (2010), Talk Talk Talk (2011) na Unpologetic (2012), kisha akapumzika na kutoa albamu ya mwisho, ANTI (2016).

"Najivunia albamu hizo kwa kweli, hadi sasa nimeuza rekodi zaidi milioni 250 na ndiye msanii wa pili wa kike duniani niliyeuza zaidi kwa muda wote, nimeshinda tuzo tisa za Grammy na ninashikilia rekodi sita za dunia," Rihanna alimueleza Harmonize.

Ghafla nazinduka kutoka usingizini, ndoto yangu nayo inakata, nasogeza mkono karibu na kitanda na kuwasha redio, nasikia wimbo wa Harmonize ambao siujui, mtangazaji anasema ni wimbo mpya kutoka katika albamu mpya ya Harmonize, Visit Bongo.

Ndipo nafahamu kumbe Harmonize ametoa albamu mpya ambayo ni ya nne kwake, amefanya kama alivyoshauriwa na Rihanna katika ndoto yangu, ametoa albamu mfululizo tangu mwaka 2022 na sasa kinachongojewa na matokeo makubwa ya kazi hizo.

Utakumbuka Harmonize alianza na albamu ya Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022) na Visit Bongo (2023), kwa zaidi ya miaka 15 sasa hakuna msanii Bongo ameweza kutoa albamu hivyo kila mwaka kama yeye.

Kwa matokea hayo, Harmonize anaingia katika orodha ya wasanii wa Bongofleva wenye albamu nyingi akiungana na Sugu (10), Lady Jaydee (8), Nikki Mbishi (6), Soggy Doggy (5), Juma Nature (5), Professor Jay (4), Fid Q (3), Diamond Platnumz (3) n.k.