Ni kubaya Wazito FC, wamesota

Friday January 14 2022
Wazito Pic
By Sinda Matiko

NI kinaya. Hali ni mbaya kwa wazito, Wazito FC. Ukiachana na matokeo duni ya uwanjani ambayo yamegoma kunyooka, sasa klabu hiyo inayomilikiwa na bilionea Ricardo Bardoer inaripotiwa kusota.

Kipigo kizito cha wikendi cha mabao 4-2 dhidi ya wavuta mkia Vihiga Bullets kwenye mechi ya ligi kuu kilichangia tu kufafanua hali ilivyo mbaya klabuni humo kwa sasa.

Kipigo hicho kilikuwa chao cha tatu mfululizo wakikifuatisha na kingine cha mabao 4-1 dhidi ya Posta Rangers. Kabla ya hapo walifinywa na Bidco United 1-0

Matokeo hayo sasa yamewaacha kwenye hatari ya kuteremshwa daraja. Wazito katika nafasi ya 16 kwenye ligi, wakiwa na alama tisa, wakifuatiwa na Mathare wenye alama saba kisha wavuta mkia Vihiga tano.

Lakini ni kipigo cha Vihiga ndicho kimetumbua jipu la kinachoendelea ndani ya Wazito wanaonolewa na kocha mzoefu Francis Kimanzi na wachezaji wamegomea vikao vya mazoezi kuelekea mchuano wao wa Jumapili dhidi ya Nzoia Sugar.

Kocha Kimanzi amedhibitisha kutokwa na wachezaji na sasa hajui nini cha kufanya kuelekea mechi hiyo.

Advertisement

“Idadi kubwa ya wachezaji wamekuwa wakisusia mazoezi na ndio sababu matokeo yetu yamekuwa kama yalivyo. Natumai klabu itafanikiwa kupata njia mbadala ya kutatua janga hili la kifedha ili tuweze kuendelea na mipango,” ameungama Kimanzi.

Baadhi ya wachezaji vile vile wanaripotiwa kwenye mchakato wa kuihama klabu hiyo katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

Pia kunao ambao tayari wameshindwa kivumilia na kujitoa hata kabla ya kupewa barua za kuachiwa na klabu.

Hao wanajumulisha mastraika Eric Gichimu, Maurice Ojwang, wingá Cliff Nyakeya, kiungo Kevin Kimani na Vincent Oburu. Watano hawa ni baadhi tu ya waliounda kikosi cha kwanza cha Kimanzi.

Ojwang tayari amerudi kwao kijijini Kisumu baada ya maisha kuwa magumu Nairobi kufuatia klabu kushindwa kuwalipa mishahara yao.

“Sikuwa na namna, nimeshindwa kulipa kodi ya nyumba na bili zinginezo. Hadi naondoka sikuwa nimelipwa mshahara wangu wa miezi minne. Nimelazimika kurudi kijijini kujishughulisha na mishe mishe zingine nikiendelea kusaka timu nyingine,” Onyango kafichua.

Onyango anasema uongozi wa klabu umekuwa ukiwazungusha kila wanapoulizia mishahara yao.

Tulipomfuata Afisa Mkuu Mtendaji wa Wazito, Dennis Gicheru, alikaushia ishu hiyo na kudai kwamba klabu inalishughulikia.

“Naelewa kuna tatizo na tunalifanyia kazi” Gicheru kasema.

Advertisement