Ndoa kipa Starlets, Yanga Princess yavunjika

KIPA wa Harambee Starlets, Pauline Kathuruh, amekatiza kandarasi yake na timu ya Yanga Princess inayoshiriki Ligi Kuu Soka la Wanawake Tanzania baada ya makubaliano ya pande zote mbili.

Kathuruh ambaye ni kipa wa zamani wa Fountain Gates Princess pia ya Tanzania, alitia saini kandarasi ya miaka miwili ikiwa ni miezi mitatu tu baada ya kuachana na timu ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL), Gaspo Women.

Kipa huyo ameichezea Yanga Princes mechi za kirafiki tangu ajiunge nao huku timu zikijiandaa na msimu mpya unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Taarifa kutoka Tanzania zinasema, kumekuwa na sintofahamu kati yake na kocha mkuu iliyomfanya aondoke kwenye timu.

Kathuruh ambaye pia alichezea Kibra Girls Soccer, alikuwa miongoni mwa Wakenya wengine wawili waliojiunga na timu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es Salaam mwaka huu.

Yanga sasa hivi ina wachezaji wawili kutoka Kenya ambao ni beki wa kushoto Wincate Kaari kutoka Thika Queens na Foscah Nashivanda aliyekuwa anakipiga na Zetech Sparks.